Serikali yazikumbusha Kampuni za Mawasiliano Kujisajili Soko la Hisa
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amezitaka Kampuni za
Mawasiliano kukamilisha taratibu za usajili katika Soko la Hisa la Dar es
Salaam kwa kuuza asilimia 25 ya hisa zote kadri ya Sheria ya Masoko ya Mitaji
na Dhamana inavyoelekeza mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar
es Salaam, Prof. Mbarawa ametaja kampuni hizo kuwa ni zile zenye leseni za
mawasiliano zilizotolewa kabla ya tarehe 1 Julai 2016 kwa ajili ya Miundombinu
ya Mawasiliano, Huduma za Mawasiliano, na Huduma za Matumizi.
“Watoa huduma wote wa
Mawasiliano wajisajili na kuuza hisa zao kwa wananchi ndani ya mwezi wa
Disemba”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa kwa Kampuni
zilizopata leseni baada ya tarehe mosi Julai, 2016 watatakiwa kutimiza sharti
hilo la kisheria kwa kipindi kisichozidi miaka miwili tangu kusajiliwa.
Waziri Prof. Mbarawa
amesisitiza kuwa Kampuni zitakazokiuka Sheria hiyo zitachukuliwa hatua za kisheria
kupitia kifungu cha 21 (C) cha EPOCA, 2010.
Aidha, amewataka
wananchi kutumia fursa hiyo kununua hisa hizo na kuwa sehemu ya wamiliki wa
makampuni ya Mawasiliano ili kuongeza kipato na kushiriki katika maamuzi ya
kampuni hizo.
Post a Comment