Mbunge Mwamoto akitazama shughuli za ujenzi wa vyoo katika shule ya Msingi Iramba.
..........................................................
MBUNGE wa jimbo la Kilolo mkoani Iringa Venance Mwamoto amechangia zaidi ya Tsh milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha miradi mbaali mbali ya kimaendeleo ikiwemo ya ujenzi wa vyoo vya wanafunzi ,madarasa ,nyumba za walimu na Zahanati katika jimboni hilo huku akiwataka viongozi wa serikali za vijiji na kata kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa wakati na ubora .
Pamoja na kuwataka viongozi hao kusimamia ujenzi huo amesema atachukua hatua kali kwa kiongozi yeyote wa serikali ya kijiji ama kata ambaye atatafuna fedha hizo za ukamilishaji wa miradi hiyo ya kimaendeleo jimboni humo.
Mbunge huyo aliyasema hayo jana wakati alipofanya ziara ukaguzi wa miradi 9 inayoendelea kwa nguvu za wananchi na Halmashauri ya wilaya ya Kilolo na kueleza kuvutiwa na miradi hiyo japo kunahitajika msukumo wa haraka katika umaliziaji wa miradi hiyo hasa ile ya vyoo vya wanafunzi ili kuwawezesha wanafunzi hao pindi shule zinapofunguliwa kuwa na vyoo bora.
Alisema kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya kwa mvua kuchelewa kunyesha katika maeneo mbali mbali ya wilaya ya Kilolo tofauti na miaka mingine ameona ni vema kuwapunguzia makali ya michango wananchi wake na badala yake sehemu ya michango ambayo walipaswa kuchangia ili kukamilisha miradi hiyo kuibeba yeye kupitia mfuko wa jimbo kwa kuchangia fedha hizo.
Kwani alisema ni rahisi kwa wananchi kuchangia nguvu zao kwa kushirikia katika ujenzi huo wa miradi hiyo kuliko kushiriki kutoa fedha jambo ambalo kwa wananchi hao ni sawa na kuwatesa kutokana na wengi wao waliuwa wakiishi kwa kutegemea kilimo na hadi sasa matumaini ya kupata fedha kwa njia ya kilimo yametoweka baada ya mvua kushindwa kunyesha .
"Ninawaombeni sana wananchi wangu kwa sasa ninyi mshiriki zaidi katika maendeleo kwa kuchangia nguvu zenu na mimi niwaunge mkono kwa kuchangia fedha ili kuifanya miradi hii ikamilike kwa wakati"
Hata hivyo alisema kuna baadhi ya maeneo wananchi wanachangamoto kubwa ya barabara hasa zile zilizopo chini ya Halmashauri kuwa barabara hizo zitafanyiwa matengenezo na ile ya Tanrod kutoka makao makuu ya wilaya ya Kilolo hadi Ndiwili mpakani mwa jimbo la Kalenga inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami mapema mwakani na kuwa kuanzia January ujenzi huo utaanza kwani barabara hiyo ipo katika ilani ya uchaguzi ya CCM.
Mbunge Mwamoto alisema kuwa kwa suala la ujenzi wa Zahanati na vituo vya afya wananchi wamejitahidi kwa maeneo mbali mbali aliyopita kukagua ujenzi umefikia hatua nzuri na kutolea mfano ujenzi wa Zahanati ya Masege ambao jengo lake bado kuezekwa na nyumba ya mganga ipo katika hatua ya kuanza kupandisha kuta kuwa kukamilika kwa Zanahati hiyo kutawawezesha wananchi hao ambao walikuwa wakilazimika kufuata matibabu Kibengu na Usokami wilaya ya Mufindi wataweza kutibiwa katika Zanahati hiyo.
Alisema katika ziara yake hiyo aliyoambatana na wajumbe wa mfuko wa jimbo kupitia fedha za mfuko wa jimbo Kijiji cha Mdeke ambako kuna ujenzi wa vyoo vya wanafunzi amechangia Tsh milioni 1 na kwenye ujenzi wa nyumba ya mwalimu amechangia Tsh milioni 2 , sekondari ya Ipeta kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya wanafunzi amechangia Tsh milioni 2, shule ya Msingi Kidabaga amechangia Tsh milioni 3 kwa ajili ya vyoo na nyumba ya mwalimu ,Wangama amechangia Tsh milioni 1 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa ,Kitongoji cha Ifiga amechangia Tsh milioni 1 kwa ajili ya kuanzisha mkondo B wakati ujenzi wa Zahanati na nyumba ya Mganga Masege amechangia Tsh milioni 5
Mbunge Mwamoto alisema ujenzi wa kituo cha Afya Ukumbi amechangia Tsh milioni 2 na katika ujenzi huo nguvu za wananchi ni Tsh milioni 35 na Halmashauri ni Tsh milioni 10 huku ujenzi wa vyumba vyamadarasa shule ya Msingi Italula amechangia Tsh milioni 2 hata hivyo alisema atafanya ziara ya ukaguzi na uchangiaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo zima ili kupitia mfuko huo wa jimbo miradi yote iweze kupata mgao huo. |
Post a Comment