Wafanyakazi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),
wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa katika uzinduzi wa Baraza jipya la Chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
...............................
Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), kimetakiwa kuchangamkia fursa za kuandaa wataalam wa kada
mbalimbali za usafirishaji wa anga ili kuinua sekta hiyo na kuiwezesha nchi
kujulikana Kimataifa.
Akizungumza jijini Dar
es Salaam katika uzinduzi wa Baraza la Chuo hicho, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa kuzalisha wataalam pekee
haitoshi bali ni jukumu la uongozi wa Baraza hilo kuhakikisha wanawasaidia
wataalam hao kwa kuwaunganisha na mashirika makubwa ya usafirishaji lengo ni
kuwajengea uwezo na kuwatambulisha kimataifa.
“Tayarisheni wataalamu
na muwakutanishe na Wakurugenzi wakuu wa Makampuni kama Emirates, Qatar na
Etihad ili kuwawezesha kupata fursa kirahisi na wao kuweza kuonekana
kimataifa”, amesema Profesa Mbarawa.
Ameongeza kuwa Chuo
kinahitaji kuchukua wafanyakazi kutoka Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ili
kutoa mafunzo kwao kwa ajili ya kuzalisha wataalam wenye ujuzi na uwezo wa
kujenga miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Guage).
“Msipotumia fursa kama
hizi za kuandaa wataalamu wa mbalimbali, tutakosa watalaamu wazawa wa miradi
mikubwa na kuanza kulalamika kuwa Chuo kipo lakini hakithaminiki kumbe mwanzoni
tulishindwa kujipanga”, amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa
amelipongeza baraza lililopita kwa uwezo mkubwa wa kukusanya mapato ya ndani
yatokanayo na ada za wanafunzi kutoka Bil. 2.1 kwa mwaka wa fedha 2011/2012
hadi kufikia Bil. 5.1 mwaka 2015/2016.
Aidha, Prof. Mbarawa ameutaka
uongozi wa Chuo hicho kuweka mifumo imara ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), ili kuweza kuwajengea mazingira mazuri kati ya Walimu na
Wanafunzi.
Sambamba na hilo,
ameutaka uongozi kupunguza idadi ya kozi zinazotolewa chuoni hapo na kuwa na
kozi chache zenye tija na soko kimataifa ili kukifanya chuo hicho kuwa cha
kipekee Afrika.
Kwa upande wake
Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo Prof. Bavon Nchomba amemhakikishia Waziri huyo
kushughulikia changamoto zote zinazoikabili chuo hicho kwa kuanzia na
upunguzaji wa idadi za kozi zisizo na tija.
Naye, Mkuu wa chuo
hicho Prof. Zakaria Mganilwa amesema chuo hicho kitaendelea kuandaa wataalamu
mahiri na waliobobea katika Sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji na kuomba
Serikali kuendelea kusaidia kuboresha miundombinu ya chuo hicho.
|
Post a Comment