Bondia FRANCIS CHEKA afungiwa Kwa miaka Miwili
Na Lilian Lundo,
MAELEZO
KAMISHENI ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBC) imemfungia Bondia Francis Cheka kushiriki katika mchezo wa ngumi kwa kipindi cha miaka miwili na kulipa faini ya shilingi laki tano kwa kitendo cha kukacha pambano baina yake na Bondia Abdallah Pazi (Dulla Mbabe).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Msaidizi wa TPBC, Chatta Michael alisema kamisheni hiyo ilitoa kibali cha pambano kati ya Cheka na Abdallah Pazi lakini bondia huyo hakufika katika pambano hilo huku akiwa ameshalipwa kiasi cha shilingi milioni tatu.
Chatta alisema kuwa Cheka aliaharisha pambano hilo lililokuwa lifanyike katika ukumbi wa Sabasaba tarehe 25 Desemba mwaka huu pasipo na kutoa taarifa, wakati Promota wa pambano hilo alikwishaingia gharama mbalimbali za maandilizi ya pambano hilo.
“Kamisheni imejiridhisha kuwa kiasi cha shilingi milioni tatu kilitolewa kwa Francis Cheka kabla ya pambano, hivyo alitakiwa apatiwe kiasi kilichobaki baada ya pambano kama alivyokubali na kusaini mkataba wa pambano hilo,” alifafanua Chatta.
Aliongeza kuwa kitendo cha kutotii makubaliano na kuchukua fedha bila kuifanyia kazi si jambo la kawaida kwa kuwa lina madhara makubwa katika kuendeleza mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.
Kwa mujibu wa Chatta alisema TPBC imetoa adhabu hiyo ili kuwa fundisho kwa mabondia wengine ambao wanaweza kusababisha mchezo wa ngumi kupoteza uaminifu kwa wakuzaji na kusababishha uvunjifu wa amani kwa watazamaji iwapo wataendelea kudanganywa kuhusu uwepo wa mapambano hewa.
Kwa upande wake, Rais wa TPBC,Chaurembo Palasa alisema adhabu hiyo ni mwanzo wa kuboresha mchezo wa ngumi za kulipwa kwani mchezo huo umekuwa ukiendeshwa bila kufuata sheria, kanuni na taratibu kwa muda mrefu.
Post a Comment