ANNA ABDALLAH afurahishwa na Ongezeko la Nafasi ya Wanawake Katika Jamii
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Aliyekuwa Mbunge wa viti maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Anna Abdallah amefurahishwa na kuongezeka kwa nafasi ya wanawake katika jamii kwa kuhusishwa katika vyombo mbalimbali vya maamuzi ya nchi.
Mbunge mstaafu huyo ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii juu ya maendeleo na nafasi ya wanawake ndani ya miaka 55 toka Tanzania imepata Uhuru mnamo mwaka 1961.
Mama Anna Abdallah amesema kuwa katika miaka ya nyuma nafasi nyingi za maamuzi katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi zilikua zikiongozwa na wanaume pekee hali iliyosababisha wanawake kuwa nyuma katika suala zima la maendeleo hivyo kupitia mashirika mbalimbali yaliyokuwa yakipigania haki sawa kwa wote yalifanya wanawake kujitambua na kufahamu umuhimu wao.
“Wanawake wameelimika wanashika nyazfa mbalimbali na wanazitumia ipaswavyo kwa kutoa mawazo chanya yenye kuleta maendeleo, ni jambo la kufurahisha kuona jamii imekubali mabadiliko haya kwa kuwaruhusu wanawake wapaze sauti zao katika utatuaji wa changamoto mbalimbali,” alisema Mama Anna.
Ameongeza kuwa kwa kutambua nafasi zao katika jamii, wanawake waliopata nafasi ya kushika nyazfa mbalimbali wako mstari wa mbele katika kufanya jitahida za kupinga mila na desturi potofu zilizopo katka jamii mbalimbali zikiwemo za kupiga vita ukeketaji, unyanyasaji wa wanawake na watoto, mimba na ndoa za utotoni pamoja na uzazi salama.
Aidha, Mama Anna ameongelea nafasi ya mwanamke ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imepiga hatua kubwa sana kwa sababu kulikuwa na idadi ndogo ya wawakilishi wanawake katika Bunge hilo kwani wanawake walikuwa hawapewi nafasi ya kuchaguliwa kwa dhana ya kuwa hawawezi uongozi.
Amefafanua kuwa baadae Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Afrika ya Kusini (SADC) ilipitisha azimio la maendeleo ya wanawake ambapo waliamua mabunge yote ya nchi wanachama kutenga asilimia 10 kwa ajili ya wabunge wanawake, kufikia hapo ndipo Serikali ya Tanzania iliona namna nzuri ya kuwashirikisha wanawake kwa kuwateua kuwa wabunge wa viti maalumu ili nao waweze kujumuika na kutoa mawazo yao katika kuendeleza nchi.
“Miaka ya sasa idadi ya wanawake wa viti maalumu imeongezeka na ni jambo la maendeleo kuona kuwa hata wanawake wa vyama vingine nao wanapata nafasi za ubunge, imeonekana kuwa wanawake wa viti maalum wakienda kugombea katika majimbo yao wanashinda kwa vishindo hiyo yote ni kwa sababu kazi zao zinaonekana wakiwa katika viti maalum,”aliongeza Mama Anna.
Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015, idadi ya Wabunge wanawake Viti Maalumu ilikuwa 113, Wabunge wa Majimbo 25 na wa kuteuliwa 2 ambapo kwa mwaka 2016 hadi 2020 Wabunge wanawake wa Majimbo ni 21 na Viti Maalum 127 wakati walioteuliwa na Mhe. Rais 3 na waliotoka Baraza la wawakilishi Zanzibar 2.
Ametoa rai kwa wanawake kuacha kusubiri nafasi za kuteuliwa na badala yake waonyeshe jitihada zao katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi zinazotangazwa katika mashirika na taasisi mbalimbali nchini.
Post a Comment