Header Ads

Serikali yalitaka Gazeti la DIRA YA MTANZANIA kukanusha Tuhuma Dhidi ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi OMBENI SEFUE

mwb1
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw.Assah Mwambene (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)  leo jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa za upotoshaji zilizotolewa na Gazeti la Dira ya Mtanzania la tarehe 29/02/2016 kuhusu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa Vyombo Habari, Bw.Jamal Zuberi na Mkurugenzi Msaidizi Habari Bw.Vicent Tiganya wote kutoka Idara ya Habari (MAELEZO).
mwb2
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia taarifa iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Bw.Assah Mwambane (ambaye hayupo katika picha) iliyokuwa ikiutaka uongozi wa Gazeti ya Dira Mtanzania kukanusha habari waliyoitoa hivi karibuni iliyokuwa na kichwa cha habari “Uchafu wa Ombeni Sefue Ikulu”.
Na Anitha Jonas – MAELEZO
………………………………………
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw.Assah Mwambene ameutaka uongozi wa Gazeti la Dira ya Mtanzania kukanusha haraka na kuiomba radhi Serikali na   Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kutokana na taarifa waliyoitoa katika toleo namba 404  la tarehe 29/02/2016 lenye  kichwa cha habari “Uchafu wa Ombeni Sefue Ikulu.
Hayo  yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi huyo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu taarifa kuwa hazikuwa na ukweli wowote kwani Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue hakuhusika katika uteuzi wa Mkurugenzi wa MSD wala kuhusika na kampuni ya CRJE katika utoaji wa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma Oktoba 2007  kwani katika kipindi  hicho alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
“Serikali inautaka uongozi wa Gazeti la Dira ya Mtanzania ukanunushe taarifa hiyo kwa uzito ule uliyotumika kuchapisha habari hiyo na kama wanapinga wakidai wana ushahidi basi waupeleke mara moja kwenye vyombo vinavyohusika  ikiwemo Sekretarieti ya Maadili na TAKUKURU”,alisema Bw.Mwambene.
Aidha,  Bw.Mwambene amesema gazeti hilo liliandika kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue alipigia chapuo Kampuni ya “UGG”  iliyowahi kuonyesha nia ya kujenga reli ya Kati nchini. Taaarifa hii pia siyo ya kweli na hakuna kampuni  yenye jina la “UGG” ilishawahi kuonyesha nia ya kujenga reli hiyo.
Mkurugenzi aliendelea kusema kuwa gazeti hilo lilimtuhumu pia Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue kuhusika na kumsafisha Bwana Eliakim Maswi wakati alichokifanya Balozi Sefue ilikuwa ni kusoma matokeo ya uchunguzi ambao hakuufanya yeye. Waliomsafisha ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Kamati ya Uchunguzi iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu kwani ndio waliiyofanya uchunguzi huo.
Hata hivyo serikali imewashauri wamiliki wa vyombo vya habari,wachapishaji,wahariri, na waandishi wa habari wajikite kwenye weledi na ukweli pia wafanye  utafiti wa kina  na kuandika mambo waliyo na uhakika nayo

No comments

Powered by Blogger.