Katibu Mkuu Kiongozi OMBENI SEFUE, kuwa Mgeni Rasmi Mkutano wa Wadau wa Takwimu
.......................................
KATIBU Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue kesho anarajia kuwa Mgeni Rasmi katika
mkutano wa wadau wa takwimu ulioandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa
ajili ya kukubaliana jinsi ya kushirikiana katika kuhakikisha takwimu za viashiria
vya Mpango wa Maendeleo Endelevu zinapatikana kwa wakati.
Akizungumza na
wandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa ofisi hiyo, Veronica Kazimoto
amesema mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Habour View, Dar es
Salaam ukiwa na lengo la kuelimishana juu ya kukamilika kwa utekelezaji wa
Malengo ya Milenia (MDGs) na kuanza kwa Malengo mapya ya Maendeleo Endelevu - Sustainable
Development Goals (SDGs).
“Kama mnavyofahamu utekelezaji
wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia - MDGs ulikuwa ni wa miaka 15 kuanzia mwaka
2000 hadi 2015. Mpango huu wa MDGs unakamilika mwaka huu na kuanza kwa mpango
mpya wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambao pia ni miaka 15 ijayo”,
amesema Kazimoto.
Kazimoto amefafanua
kuwa mkutano huo utahudhuriwa na wadau wa takwimu takribani 100 kutoka Wizara,
Idara, Wakala na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Wadau wa Sekta
Binafsi pamoja na Wadau wa Taasisi za Elimu ya Juu.
Aidha, Afisa Habari
huyo amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeandaa mkutano huo kwa kuwa ndio yenye
mamlaka nchini ya kutoa takwimu rasmi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo
na kufanya maamuzi sahihi.
Kazimoto ameongeza
kuwa mwezi Septemba mwaka huu, viongozi wa nchi mbalimbali duniani akiwemo Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, walikutana
nchini Marekani kwa ajili ya kutathmini utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia
– MDGs ambapo ilionekana kwamba kuna baadhi ya malengo yalikuwa yamefanikiwa na
mengine hayakufanikiwa.
Kutokana na hali hiyo,
viongozi hao walikubaliana na kuridhia mpango mbadala wa MDG ambao unaitwa Mpango
wa Maendeleo Endelevu ambao pia ni wa miaka 15 kuanzia 2015 hadi 2030.
Mkutano huo wa viongozi mbalimbali duniani
uliidhinisha mpango huo mpya wenye malengo
17 na viashiria 169 ambavyo kila nchi kwa uratibu wa Kitengo cha Takwimu cha
Umoja wa Mataifa inatakiwa kuvipitia na kuona kama kuna takwimu za kutosha
kukidhi upimaji wa malengo kwa kutumia viashiria hivyo.
Malengo hayo 17
yaliyoidhinishwa na mkutano huo
wa
wakuu wa nchi mbalimbali duniani ni pamoja na Kuondoa Umaskini wa aina zote, kuondoa njaa, kuhakikisha
kuna maisha yenye afya bora na kuhamasisha ustawi kwa wote, Kulinda uhai wa
viumbe juu ya ardhi, elimu Bora na usawa wa kijinsia.
Malengo mengine
ni kuhakikisha upatikanaji na matumizi endelevu ya maji na usafi wa mazingira
kwa wote, kuhakikisha kuna upatikanaji wa huduma rahisi ya nishati endelevu na
ya kisasa kwa wote, uwepo wa Ajira na ukuzaji wa uchumi, uwepo wa Viwanda na Miundombinu,
kulinda Amani na Utawala wa Sheria na kupungunza tofauti ya kipato baina ya
nchi na nchi na ndani ya nchi.
Ameyataja malelengo
mengine kuwa ni pamoja na uwepo wa Miji na Jamii endelevu, kuwajibika katika Uzalishaji,
kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na madhara
yake, kutunza na kuwa na matumizi endelevu ya bahari pamoja rasilimali za
baharini kwa ajili ya maendeleo endelevu na kushirikiana na wadau katika
kufikia malengo ya SDGs.
Post a Comment