SEIF SHARIF HAMAD ahitimisha Kampeni zake Mjini UNGUJA
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia katika mkutano wa kufunga kampeni za Chama hicho kwa Zanzibar katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar. |
Wafuasi na wapenzi wa CUF chini ya mwamvuli wa Ukawa, wakifuatilia mkutano huo wa kufunga kampeni katika viwanja vya Maisara. |
Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema Mhe. Juma Duni Haji, akihutubia kwenye Mkutano huo. |
Makamu Mwenyekiti
wa Timu ya Kampeni ya CUF Mansour Yussuf Himid, akizungumza katika mkutano huo.
(Picha na Salmin Said, OMKR) |
Na:
Hassan Hamad,Unguja
Chama Cha Wananchi
CUF kimefunga rasmi kampeni zake za uchaguzi kwa upande wa Zanzibar na kuwataka
wadau wa uchaguzi kuheshimu maamuzi ya wananchi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Jumapili ijayo.
Akizungumza kwenye
mkutano huo wa ufungaji wa kampeni uliofanyika viwanja vya Maisara Mjini
Zanzibar, Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif
Hamad, amesema wananchi ndio wenye mamlaka ya kuiweka Serikali madarakani,
hivyo maamuzi watakayoyafanya kwenye uchaguzi huo hayana budi kuheshimiwa.
Amerejea kauli yake
ya kukubali matokeo iwapo uchaguzi utafanyika kwa uwazi, huru na haki na
kuwashauri wagombea wengine wa Urais kutoa kauli kama hiyo ili kuwaondoshea
hofu wananchi.
Hata hivyo amesema
hatoridhia matokeo iwapo atashinda uchaguzi huo, na kuelezea matumaini yake ya
kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao.
Aidha amesema
atatumia uwezo wake kuviimarisha vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
na hana nia ya kumfukuza kiongozi yoyote wa vikosi hivyo.
Amemshauri Rais
Kikwete na Dkt. Shein kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi ili kuhakikisha kuwa
uchaguzi ujao unafanyika katika hali ya Amani na usalama.
Amesema uchaguzi usiwe sababu ya kuvurugika
kwa amani iliyopo na kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu kuhakikisha kuwa
amani iliyopo inalindwa.
Amewataka wananchi
kuondosha hofu wanapokwenda kupiga kura na kumchagua kiongozi wanayemtaka, na
kwamba hakuna mwananchi atakayefuatiliwa au kujulikana taarifa zake.
Nae Mgombea Mwenza wa
Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema Mhe. Juma Duni Haji
amesema ana imani kuwa Watanzania wako tayari kwa mabadiliko.
Amesema iwapo wananchi
watawachagua wagombea wanaotokana na Umoja wa Ukawa wataendeleza maridhiano na
umoja wa wananchi, sambamba na kurejesha katiba iliyopendekezwa na wananchi
ambayo itato haki kwa wananchi wote.
Kwa upande wake
Makamu Mwenyekiti wa Timu ya Kampeni ya CUF Mansour Yussuf Himid, amewataka
wananchi kumchagua Maalim Seif ili aweze kuleta mabadiliko ya kiuchumi nchini.
Amesema
Maalim Seif ni kiongozi anayejiamini, jasiri na mwenye uwezo wa kuongoza nchi,
na kwamba iwapo wazanzibari watafanya maamuzi sahihi watajionea mabadiliko kwa
kipindi kifupi baada ya uchaguzi.
Post a Comment