Header Ads

Maadhimisho Siku ya Takwimu Yafanyika

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Takwimu Duniani yaliyofanyika leo katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni "Takwimu Bora, Maisha Bora".
Wanafunzi wa Stashada wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika wakiwa wameshikilia bendera za nchi wanachama wanaoshikiana na nchi ya Tanzania kuendesha chuo hicho wakati wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Duniani yaliyofanyika leo katika Chuo hicho kilichopo jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni "Takwimu Bora, Maisha Bora".
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa (hayupo pichani) wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Takwimu Duniani yaliyofanyika leo katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni "Takwimu Bora, Maisha Bora". 

Na: Veronica Kazimoto, Dar es Salaam

WATAKWIMU vijana wameaswa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kusaidia katika ukusanyaji na upatikanaji wa takwimu bora zitakazosaidia katika kupanga mipango ya maendeleo.
 
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Takwimu Duniani yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema vijana wenye taaluma ya takwimu wana nafasi kubwa katika kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji wa takwimu bora nchini.

"Ninyi watakwimu ambao bado ni vijana mna jukumu la kuhakikisha kuwa mnatumia taaluma yenu ya takwimu katika kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi ili zitumike katika kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo,” amesema Dkt. Chuwa.

Dkt. Chuwa amesema maadhimisho haya ya Siku ya Takwimu Duniani yana nafasi kubwa katika kutambua umuhimu wa takwimu katika kufanikisha utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kuboresha maisha ya wananchi.
 
Aidha, amesema kuwa kutokana na dunia kuzindua Mpango Mpya wa Maendeleo Endelevu (SDGs), ofisi yake imejipanga vyema katika kuhakikisha takwimu bora zinapatikana kwa wakati ili zisaidie Taifa katika kutekeleza malengo ya mpango huo.

“Kutokana na umuhimu wa takwimu katika utekelezaji wa malengo 17 na viashiria 169 vya Mpango wa Maendeleo Endelevu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imejipanga vyema katika kuhakikisha takwimu zote muhimu zinapatikana na kusaidia katika utekelezaji wa malengo ya mpango huu,” amesisitiza Dkt. Chuwa.

Siku ya Takwimu Duniani huadhimishwa kila baada ya miaka mitano tarehe 20 Oktoba ambapo kwa mwaka huu maadhimisho haya yameongozwa na Kauli mbiu isemayo “Takwimu Bora, Maisha Bora”.

No comments

Powered by Blogger.