Maalim SEIF SHARIF HAMAD ajinadi kwa Wananchi Katika Jimbo la MKWAJUNI
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi wa chama hicho katika viwanja vya jimbo la Mkwajuni. |
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi kadi kwa mmoja kati ya vijana 39 wa jimbo la Mkwajuni waliojiunga na CUF. |
Wafuasi na wapenzi wa CUF wakifuatilia mkutano huo. |
Na:
Hassan Hamad (OMKR)
Mgombea Urais wa
Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema anakusudia
kuuzindua rasmi mpango wake wa kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika
Mashariki mwishoni mwa wiki hii.
Amesema
anapozungumzia mpango huo huwa hafanyi utani bali anazungumza akiwa na mikakati
maalum ya kuweza kuibadilisha Zanzibar kufikia lengo hilo.
Maalim Seif ambaye
pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa kauli hiyo wakati
akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Mkwajuni Mkoa
wa Kaskazini Unguja.
Amesema tayari chama
hicho kimeshapanga mikakati imara ya kuweza kuikomboa Zanzibar kiuchumi katika
kipindi kifupi kijacho iwapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar.
Akizungumzia
mafanikio ya safari yake ya kichama nchini Afrika ya Kusini, amesema alikutana
na viongozi wa makampuni mbali mbali ya nchi hiyo ambao walikubali kushirikiana
nae kuikomboa Zanzibar kiuchumi iwapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi
mkuu ujao.
Kuhusu matarajio ya
ushindi kwa chama hicho Maalim Seif amesema kina matarajio makubwa ya kupata
ushindi na kuapa kuwa hakuna atakayeweza kuzuia mabadiliko hayo.
Amesema wananchi wa
Zanzibar wameshajiika kuleta mabadiliko na kuwahimiza kujitokeza kwa wingi
kupiga kura ili kuweza kufikia malengo hayo.
Ameishauri Tume ya
uchaguzi ya Zanzibar kujiandaa kutoa matokeo ya uchaguzi mapema, ili kuzuia
vurugu zinazoweza kuepukika.
“Inawezekana kabisa
kutoa matokeo siku hiyo hiyo kwa majimbo 54 ya Zanzibar. Naamini kuwa ikifika
saa sita za usiku matokeo yote ya Zanzibar yatakuwa yamekamilika, hivyo Tume
wajitahidi wayatangaze ili wananchi wapate kutulia” alieleza.
Maalim Seif
amesisitiza haja ya kuwepo kwa uchaguzi wa amani, na kuwata vijana wa chama
hicho wasikubali kuchokozeka na kupelekea kuvunjika kwa amani ambayo ni hazina
kubwa kwa taifa.
Kuhusu Masheikh wa
Jumuiya ya Uamsho wanaoshikiliwa Tanzania Bara, Maalim Seif amesema siku zao za
kukaa ndani sasa zinahesabika kwani iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar
atawarejesha masheikh hao Zanzibar ndani ya kipindi cha wiki moja baada ya
kuapisha.
Nae Naibu Katibu Mkuu
wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema iwapo Maalim Seif atachaguliwa kuwa
Rais wa Zanzibar, atayarejesha yale yote yaliyoahidiwa na Marehemu Mzee Abeid
Amani Karume, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za elimu na afya bila ya malipo.
Mjumbe wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo Janeth Fussi akizungumza katika mkutano huo amesema
Maalim Seif anatosha na anavyo vigezo vyote vya kuchaguliwa kuwa Rais wa
Zanzibar.
Post a Comment