Tamasha la Sanaa na Utamaduni Kufanyika Bagamoyo Septemba 21 hadi 27, 2015
Mwenyekiti wa Tamasha la 34 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni, John Mponda (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu tamasha hilo litakalofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 27, 2015 katika Kumbi na Viunga vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), mkoani Pwani. Kulia ni Katibu wa Tamasha hilo na Ofisa Biashara, Benjamini Malimbali na Ofisa Habari, Sophia Mtakajimbo.
Hapa Mwenyekiti wa Tamasha hilo, John Mponda (kulia) akisisitiza jambo kuhusu tamasha hilo. Kushoto ni Ofisa Habari wa Tamasha la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
.....................................................................
.....................................................................
TAMASHA la
kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo liliasisiwa mwaka 1981 na Chuo cha
Sanaa Bagamoyo ambacho kwa sasa ni Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo.
Lengo kuu la Tamasha kwa wakati huo ilikuwa ni kuwapa nafasi wanafunzi wa chuo
cha sanaa kuonyesha kwa vitendo yale waliojifunza kwa mwaka mzima kwa
kuwashirikisha wakazi wa Bagamoyo, baada ya Tamasha hilo kufanikiwa uongozi wa
chuo uliamua tamasha hilo lifanyike kila mwaka kwa kushirikisha Vikundi mbalimbali
vya ndani na nje ya nchi ili kubadilishana Uzoefu na hivyo kujizolea umaarufu ndani na nje ya
Tanzania.
Tamasha la
kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo mwaka huu litafanyika kwa mara ya 34
kuanzia tarehe 21-27 Septemba katika kumbi na viunga vya Taasisi ya Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo ambao ndio wenyeji na waandaaji wa tamasha hilo kongwe
Tanzania.
Maandalizi yote
ya Tamasha hili yamekamilika Tamasha la mwaka huu linabeba Kauli mbiu isemayo ‘SANAA
NA UTAMADUNI KATIKA UCHAGUZI HURU NA WA AMANI’ Aidha kutakuwa na mada ndogondogo
zitakazotolewa kupitia kongamano na warsha zitakazohusu Haki za binadamu, Rushwa na kupinga Mauaji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino)
Mgeni rasmi
katika ufunguzi wa Tamasha atakuwa mzee Rashid Masimbi, aliyekuwa mkuu wa chuo
wa kwanza toka taasisi ilivyokuwa chuo cha sanaa,hivyo kwa kutambua mchango
wake kwenye sanaa Taasisi imempa heshima ya kuwa mgeni rasmi .
Tamasha la mwaka
huu litahusisha Ngoma za Asili, Maigizo, Sarakasi, Mazingaombwe, Muziki wa
kisasa na asili, Sanaa za Ufundi na
bidhaa mbalimbali.
Jumla ya vikundi
65 kutoka ndani na nje ya Tanzania vimethibitisha kushiriki,ambapo vikundi
59 ni kutoka ndani ya Tanzania na
vikundi 6 kutoka nchi za Kenya, Namibia, Afrika Kusini, Korea na Congo na
Zimbabwe.
Kiingilio kwenye
tamasha kwa wakubwa shilingi 3000/=,kwa watoto shiling 1000/= na kwa wageni
wasio watanzania shilingi 5000/=
Taasisi inatoa
wito kwa wadau mbalimbali wa Sanaa,Makampuni,Taasisi za Serikali na zisizo za
Serikali kujitokeza kudhamini tamasha hili muhimu ambalo hufanyika kila mwaka
ili kulifanya liwe bora na la kimataifa zaidi , kwa mustakabali wa sanaa na
utamaduni wa Mtanzania.
Post a Comment