Mfumo wa Usajili na Uhifadhi wa Takwimu za Matukio ya Binadamu Kuanzishwa, TANZANIA BARA
....................................................... |
Na Veronica Kazimoto
Usajili wa Raia una jukumu la
msingi katika kutekeleza matakwa ya utawala bora na maendeleo ya kiuchumi
katika taifa lolote lile duniani.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Sheria na Katiba Maimuna Tarishi wakati akifungua mkutano wa wadau
wa kujadili Rasimu ya Mkakati wa Usajili na Uhifadhi wa Takwimu za Matukio
Muhimu ya Binadamu uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Tarishi amesema Usajili wa Raia
ni wajibu wa kisheria kwa kuwa unasaidia katika upangaji wa mipango madhubuti
ya maendeleo pamoja na kuiletea maendeleo jamiii kulingana na Mkakati wa
Kuondoa Umaskini na Kukuza Uchumi Tanzania (KUKUTA II).
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya
Katiba na Sheria amebainisha kuwa mfumo wa Usajili wa Raia uliopo sasa Tanzania
Bara umekuwa ukifanya kazi kwa kusuasua
na hivyo kusababisha baadhi ya wananchi kutotambulika katika kumbukumbu rasmi
za kiutawala.
“Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na
Makazi iliyofanyika mwaka 2012, ni asilimia 15 tu ya watanzania ndio
waliosajiliwa na kupata vyeti, hali inayowaacha wengi pasipo kutambulika popote
katika kumbukumbu rasmi za kiutawala,” amesema Tarishi.
Ameongeza kuwa usajili ya vifo
ndio uko katika hali mbaya zaidi ambapo ni matukio machache ya vifo
yanayoandikishwa na sababu za vifo hivyo hazibainishwi kwa usahihi au
hazibainishwi kabisa hali inayosababisha ugumu katika kutekeleza majuku kwa
upande wa sekta ya afya nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa ambaye ofisi yake ni mdau muhimu
wa mfumo huu, amesema lengo la mkakati huu ni kuanzisha mfumo wa Usajili wa
Raia ambao unakidhi vigezo vya kimataifa ambao ni wa kudumu na unaofikia watu
wote katika kusajili matukio muhimu ya binadamu na kuzalisha takwimu za matukio
hayo katika namna ambayo ni endelevu na ya kuaminika.
Dkt. Chuwa amesema mfumo huu wa
Usajili wa Raia ukikamilika utasaidia kupata huduma zote za usajili katika sehemu
moja kwa vituo vyote vya usajili nchini.
Nae Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) Emmy Hudson amesema mfumo uliopo
sasa uko mbali na wananchi walio wengi hasa wa maeneo ya vijijini kwasababu ngazi
ya chini ya usajili ni ofisi ya Katibu
Tawala wa Wilaya.
Changamoto hii na nyingine inasababisha huduma hii ya usajili kutofika kwa urahisi
kwa wananchi walio wengi hali ambayo inaleta uhitaji wa mabadiliko ambayo ili
tufanikiwe, RITA inahitaji peke yake haitamudu kuzikabili changamoto za mfumo
pasipo kuhusisha wadau mbalimbali katika kuboresha mfumo huu.
Usajili wa Raia ulianzishwa na sheria ya kikoloni mnamo mwaka 1917. Kwa
mujibu wa sheria hiyo usajili ulikuwa ni lazima kwa wakazi wa Tanganyika na baada
ya uhuru, sheria hii ilirithiwa ambapo licha ya mabadiliko kadhaa ambayo
yamekuwa yakifanyika bado wananchi wamekuwa na kasumba ya kutokuona umuhimu wa Usajili
wa Raia nchini.
Post a Comment