Header Ads

JANET MBENE; Akerwa na uchakavu wa Miundombinu Maeneo ya Viwanda

 TANZANIA ni moja kati ya nchi ambayo ipo katika jitahada kubwa kuhakikisha kuwa inakuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020.

Katika kufanikisha hili Tanzania imekuwa katika mipango ya kuhakikisha kuwa kunakuwepo na viwanda vidogo na vikubwa vinavyofanya kazi kwa ajili ya kuinua uchumu wa nchi.

Kwa kipindi zaidi ya miezi mitatu nimekuwa nikiambatana  na Mhe. Janet Mbene, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara katika ziara yake ya kutembelea viwanda mbalimbali hapa nchini ili kujionea uzalishaji na uendeshaji wa viwanda hivyo.

Mbali ya kujionea mafanikio makubwa ya uzalishaji katika viwanda hivyo na jinsi ambavyo watanzania wameweza kupata ajira kupitia viwanda hivyo, bado kumekuwepo changamoto ya miundo mbinu duni ya barabara zinazoelekea viwandani. 

Mhe. Janet Mbene, anasema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto za uzalishaji bado kuna changamoto kubwa ya miundombinu katika njia za maeneo ya viwanda hali inayochangia kupunguza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.

Mhe. Mbene ameeleza kuwa sehemu kubwa ya Tanzania ambayo imetengwa kwa ajili ya viwanda imekosa miundo mbinu ya barabara ya lami na kufanywa sio kipaumbele licha ya serikali kuimba kila siku kuwa sasa imefikia hatua tuende katika uchumu wa viwanda ili nchi yetu iweze kuendelea.

“kuna tatizo kubwa sana katika Halmashauri zetu ambako huko ndipo viwanda vimejengwa, licha ya wamiliki wa viwanda kwa umoja wao kutaka kuchangia na kutengeneza barabara bado Halmashauri zetu zimekuwa zikisita kutoa ushirikiano kwa kuhitaji wapewe wao pesa ili waweze kujenga barabara badala  ya kushirikiana na wawekezaji ambao wanataka kujitolea”anasema Janet Mbene.

Anataja mfano katika Halmashauri ya jiji la mbeya kuwa wameshindwa kutoa ushirikiano kwa eneo la viwanda ambapo kiwanda cha madini cha Marmo and Granito, TBL na Pepsi wamejitolea kujenga barabara hiyo kwa gharama zao lakini bado halmashauri inataka yenyewe ndiyo ipewe pesa.


Anaongeza kuwa hali hiyo pia ipo katika Halmashauri ya mji wa Moshi mkoa wa Kilimanjaro katika barabara ya kwenda Bonite na kiwanda cha bia cha Serengeti Breweries ambao nao wako tayari kujitolea kujenga barabara lakini bado Halmashauri zinaomba zipewe pesa kwanza kwa jili ya ujenzi wa barabara hiyo.

Mbene anasemakuwa  hali hiyo pia ameikuta katika barabara ya viwandani ya mkoa wa morogoro ambayo imeshindwa kupitishwa hata greda la kuchonga ili kuweza kuweka sawa njia hiyo ya viwanda.

Nelson Mchukya ni meneja usafirishaji wa kiwanda cha Mazava Winds Group Co. kilichopo Morogoro anasema kuwa njia ya kuingia kiwandani kwao ni mbovu kiasi cha kupelekea kusimamisha uzalishaji wakati wa mvua.

Anataja kuwa mara zote wamekuwa wakiwaomba watu wa Halmashauri waweze kuwatengenezea njia nzuri japo hata kwa kuleta greda na wao kuchangia mafuta wameshindwa kufanya hivyo kwa madai kuwa wana majukumu mengine.

Mchukya anataja kuwa pindi wanapoamua kusimamisha uzalishaji athari zake ni kubwa sana kwani nchi inakosa fedha za kigeni na baadhi ya wafanyakazi hulazimika kurudishwa majumbani hivyo kupunguza kipato kwa wakazi wa eneo hilo ambao wameajiriwa na kiwanda hicho.

Anasema kuwa kiwanda kinawafanyakazi zaidi ya 1500 lakini kukitokea tatizo la uzalishaji wafanyakazi zaidi ya 1000 hulazimika kurudi nyumbani.

Hali kadhalika, Waziri Mbene aliahidi kushughulikia tatizo hilo kwa kuahidi kukutana na waziri wa TAMISEMI kuona ni namna gani wanaweza kutatua tatizo hilo kwa kuwaonya watendaji wanaotanguliza maslahi yao mbele.

Mbene anasema Serikali ipo kwa ajili kuhakikisha kuwa wananchi wake wanapata maendeleo hivyo kamwe haitokubali kuona kuwa mtu anayetaka kujinufaisha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.


 Imeandaliwa na Humphrey Shao

No comments

Powered by Blogger.