Maalim SEIF SHARIF HAMAD, akutana na Balozi wa Qatar, Sheikh ABDULLA JASSIM AL-MAADADI
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na balozi wa Qatar nchini Tanzania Sheikh Abdulla Jassim Al-Maadadi, nyumbani kwake Mbweni. |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akimsindikiza balozi wa Qatar nchini Tanzania Sheikh Abdulla Jassim Al-Maadadi, baada ya mazungumzo yao nyumbani kwake Mbweni. |
........................................................................
Qatar imesema
inakusudia kuendeleza uhusiano wa kindugu uliopo kati yake na Zanzibar,
sambamba na kukukuza mahusiano ya biashara na uchumi.
Balozi wa Qatar
nchini Tanzania Sheikh Abdulla Jassim Al-Maadadi ameeleza hayo leo alipokuwa na
mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif
Hamad, nyumbani kwake Mbweni.
Amesema Qatar na
Zanzibar zina uhusiano wa muda mrefu ambao unapwa kuendelezwa katika nyanja zote
za maisha kwa maslahi ya pande zote mbili.
Balozi Al-Maadadi
ameelezea kuridhishwa na mazingira ya Zanzibar na kuahidi kushirikiana na Jumuiya
ya wawekezaji ya Qatar, ili kuangalia uwezekano wa kuwekeza miradi yao ya
kiuchumi.
Amesema Zanzibar ni
pahala pazuri pa kuwekeza, hivyo atafanya juhudi kuona kuwa wawekezaji wa Qatar
wanaelekeza nguvu za kuwekeza visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Nae Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amumuhakikishia balozi huyo
kuwa Zanzibar ni mahala salama kwa uwekezaji.
Amesema mbali na
mazingira mazuri yaliyopo, ukarimu na utamaduni wa Wazanzibari ambao unalingana
na ule wa watu wa Qatar, unachukua nafasi kubwa kuweka mazingira bora ya
uwekezaji kwa wawekezaji wa Qatar.
Amesema Zanzibar na
Qatar zinaweza kushirikiana katika maeneo mbali mbali yakiwemo uvuvi wa bahari
kuu pamoja na utalii, huku akishajiisha utalii wa daraja la juu.
Maalim Seif ameelezea
matumaini yake kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Qatar kuja kuwekeza
Zanzibar, ambapo pia amezungumzia ziara yake aliyoifanya nchini Qatar hivi
karibuni na kukutana na viongozi wakuu pamoja na Jumuiya ya wafanyabiashara wa
nchi hiyo.
Aidha Maalim Seif
ametoa wito kwa kampuni za uchimbaji wa mafuta na gesi za nchini Qatar kukaa
tayari, kwani Zanzibar inajiandaa kutoa tenda za uchimbaji wa mafuta na gesi
katika siku za hivi karibuni.
Katika hatua
nyengine, Maalim Seif amesema serikali inakusudia kuuimarisha uwanja wa ndege
wa Pemba, ili kukifungua kisiwa cha Pemba kibiashara na utalii.
Makamu huyo wa Kwanza
wa Rais amesema kisiwa cha Pemba kimekuwa na utajiri mkubwa katika sekta ya
kilimo hasa zao la Karafuu ambalo ni tegemeo kubwa kwa wakulima wa zao hilo na
Taifa kwa ujumla, na kutoa wito wa kuendelezwa.
Sambamba
na hilo Maalim Seif amewataka wananchi kukiendeleza kilimo cha minazi, ili kuliendeleza
zao hilo la kihistoria visiwani Zanzibar kuweza kusaidiana na zao la karafuu kwa
lengo la kukuza uchumi na kipato cha wananchi.
Post a Comment