Serikali yaahidi Kutoka Kipaumbele kwa WAHANDISI Wazalendo
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akizungumza na Wahandisi kutoka maeneo mbalimbali nchini wakati wa ufunguzi wa Siku ya Wahandisi nchini mwaka 2015 jijini Dar es salaam. |
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akikabidhi vyeti na miongozo mbalimbali ya utendaji wa kazi kwa Wahandisi baada ya kuapishwa nchini leo jijini Dar es salaam. |
Na.Aron Msigwa- MAELEZO.
Serikali
imesisitiza kuwa itaendelea kuwatumia wahandisi wazalendo waliosajiliwa
na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kutekeleza miradi ya ujenzi wa
miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Wahandisi kwa mwaka 2015
leo jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue
amesema kuwa Wahandisi wanao mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi
kwa kuifanya mipango iliyo kwenye karatasi kuwa katika uhalisia
unaoonekana kwa macho.
Amesema fani ya uhandisi
inagusa maisha ya watu moja kwa moja hasa sekta ya ujenzi wa
miundombinu ya maji, umeme, majengo,miundombinu ya migodi, hospitali,
barabara, viwanda na shughuli nyingine za kihandisi.
"Ni
jambo lililowazi kuwa tuna kila sababu ya kujivunia maendeleo na
mafanikio tuliyofikia, tuna kila sababu ya kuwatumia na kutoa kipaumbele
kwa wahandisi wazalendo ,wahandisi wetu wanaweza" Amesisitiza Balozi
Sefue.
Amewataka wahandisi hao kuendelea
kuzingatia weledi pindi wanaposimamia utekelezaji wa miradi ya Serikali
ili miradi hiyo iendane na thamani halisi ya fedha za wananchi kwa kuwa
Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia miradi hiyo.
"Nawataka
muendelee kuzingatia weledi,muwe waadirifu na mfanye kazi kwa bidii ili
tufikie malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025,mkumbuke kuwa kazi
mnazofanya zinaonekana na watu wote, zikiwa mbaya au kuwa chini ya
viwango watasema tu na mtaonekana hamzingatii taaluma wala viapo vyenu"
Amesisitiza.
Amesema toka mwaka 2005 hadi 2015
Sekta ya Uhandisi nchini Tanzania imeweza kuwanufaisha watanzania kwa
kuzalisha ajira 256,480 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka
mazingira mzauri kwa kuboresha shule , vyuo na taasisi mbalimbali ili
ziweze kuzalisha wahitimu bora wenye kuhimili ushindani soko.
Aidha,
ameziagiza Halmashauri kote nchini kuhakikisha kuwa zinakuwa na
wahandisi waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi kabla ya Juni
30, 2016 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka msisitizo katika
ubora wa wahandisi wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuimarisha
ushirikiano uliopo katika sekta ya ujenzi baina Tanzania na nchi za
jirani.
Awali akiongea kabla ya kumkaribisha
mgeni rasmi kuongea na washiriki wa maadhimisho hayo Naibu Katibu
Mkuu,Wizara ya Ujenzi, Muhandisi Joseph Nyamhanga, amesema kuwa siku
hiyo inatoa fursa kwa wahandisi kote nchini kukutana na kubadilishana
uzoefu wa kitaalam katika kuleta maendeleo nchini.
Amesema
Bodi ya Usajili wa Wahandisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
imewezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo nchini Tanzania lengo kubwa
likiwa ni kuweka msukumo na msisitizo wa kutekeleza Dira ya Maendeleo ya
Taifa 2015, kuangalia changamoto na mikakati ya kukabiliana nzao.
Ameongeza
kuwa mkutano huo wa mwaka unafanyika nchini Tanzania kwa mara ya 13
ukizishirikisha baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Nigeria,Afrika
kusini,Malawi, Kenya na wawakilishi kutoka Norway.
Amefafanua
kuwa kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) sekta ya ujenzi
imetoa mchango mkubwa kupitia wahandisi waliopo nchini kwenye shughuri
za ujenzi wa miundombinu, ushauri na usimamizi wa miradi mbalimbali.
Amebainisha
kuwa kasi ya Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati inaendelea
kutekelezwa kwa kasi kupitia sekta ya ujenzi, viwanda,kilimo,
umwagiliaji na shughuli za migodini.
Ameeeleza
kuwa Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa wahandisi wazalendo na
kuweka mkazo katika kushughulikia changamoto walizonazo ili taifa
liendelee kunufaika kutokana na gharama kubwa inayotumika kuwasomesha.
"Serikali
inatumia gharama kubwa kuwasomesha wahandisi wetu, ni jambo jema
tukiendelea kuweka mkazo ili kuwalinda wahandisi wa ndani na mabadiliko
yaliyopo yanayoweza kusababisha wengi wao kutafuta ajira nje ya nchi"
Amesema.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya
Wahandisi nchini (ERB) Muhandisi Steven Mlote ameeleza kuwa maadhimisho
ya Siku ya Wahandisi nchini yanaambatana na majadiliano ya kina kuhusu
shughuli za kihandisi nchini na miaka 15 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2025.
Aidha, amesema kuwa ERB
imewatambua na kuwapa Tuzo na zawadi mbalimbali wahandisi na wahitimu wa
Taasisi waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao mwaka 2014/2015
huku baadhi ya wahandisi wahitimu wakiapa kiapo cha utii kwa taaluma
yao.
Ameongeza kuwa katiaka kipindi cha siku 2
za maadhimisho hayo kutakuwa na maonesho ya kiufundi ya jumuiya za
wahandisi wa Tanzania na taasisi mbalimbali za elimu ya Uhandisi
zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es
salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Uhandisi na Teknolojia St.Joseph , Chuo cha
Ardhi (ARU), Makandarasi ,Kampuni za Ushauri wa kihandisi,Mashirika na
makampuni ya kibiashara na taasisi za utafiti.
Post a Comment