Salma akiwa na baadhi ya wasanii aliowalipia sehemu ya Bima ya Afya. 
 
 Na Mwandishi wetu 
 
 
Jukwaa La Sanaa la BASATA wiki hii lilipata wazungumzaji wa
aina yake na kulifanya kuwa jukwaa lililochangamka na kuwa na mazungumzo ya
zaidi ya masaa matano.  
Wasanii takriban 70 walikaa wakichambua maada mbalimbali
kuhusu mustakhabari wa sanaa katika nchi yetu. Jambo ambalo liliingiza
changamoto katika jukwaa hili, ni kuweko katika meza kuu wasanii wawili ambao
walianza sanaa nchini na hatimae kuhamia ughaibuni ambako ndiko wanaishi kwa
sasa. 
 
 
Wasanii
 Salma Moshi aliyekuwa akijulikana kama Salma Nyoka,
msanii wa kwanza wa kike kuchezea nyoka katika jukwaa, na ambaye alikuwa
 kiongozi wa vikundi vilivyotamba kama DDC Kibisa Cultural Troupe Super 
Mama Cultural Troupe na Ujamaa Cultural Troupe, na Abbu Omar,
mwanamuziki aliyewahi kupigia bendi kama Urafiki na UDA Jazz ambae 
kwanza
alihamia Kenya na kupiga na kurekodi na makundi kama Simba wa Nyika na 
Les
Wanyika na pia kurekodi album kadhaa akiwa na kundi lake ambaye hatimae
alihamia Japan ambako amekuwa akiishi kwa kupiga muziki na akiwa na 
waTanzania
wengine kama Lista na Fresh Jumbe. 
 
 
Mazungumzo
 yaligusia nyanja mbalimbali ikiwemo umuhimu wa
kuwa na mikataba kabla ya kazi, kuboresha kazi ili kuweza kuuza nje, 
namna ya kujitambulisha  duniani kwa kuwa na websites na blogs, na pia 
serikali kubadilika na kuweko
mfumo wa uongozi wa sanaa kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa.  
 
Katika 
mkutano
huo, John Kitime Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanamuziki aliongelea fursa ya
 Bima
ya Afya kwa wasanii, ambapo Salma Moshi alijitolea kuwalipia nusu ya ada
wasanii wanne, na kumlipia bima kamili Mzee Kassim Mapili ambaye kwa 
sasa
anasumbuliwa na moyo na figo.  
 
Abuu Omar pia aliamua kulipia Bima yake na
 kueleza kuwa katika nchi ya Japan ni lazima kila mwananchi kuwa na Bima
 ya Afya, kwani ugonjwa hauji kwa taarifa na matibabu ni gharama kubwa. 
 
 
Mkutano huo ulianza saa tano na kulazimishwa kusimamishwa
saa kumi, kwani wasanii bado walikuwa na mengi ya kuwauliza wasanii hawa nguli
walioweza kuendeleza maisha ughaibuni kupitia sanaa. 
 | 
Post a Comment