Wananchi Jijini MBEYA Waendelea Kupatiwa Elimu Kuhusu JOTO ARDHI
Meneja
Mkuu Shirika la Uendelezaji Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC),
Mhandisi Boniface Njombe (aliyesimama) akielimisha Umma wa Kata ya Swaya
wakati walipotembelea eneo la kata hiyo ikiwa ni sehemu ya Kampeni ya
uelimishaji kuhusu manufaa ya Jotoardhi hivi karibuni mkoani Mbeya. Kushoto ni Mkurugenzi wa masuala ya Ufundi wa TGDC, Bwana Karamaeli Mnjokava.
Mkurugenzi
wa masuala ya Ufundi wa TGDC, Bwana Karamaeli Mnjokava.(aliyesimama
mbele) akichangia mada kuhusu jotoardhi na manufaa yake kwa wakazi wa
Kata ya Swaya hivi karibuni mkoani Mbeya.
Baadhi
ya Wakazi wa Kata ya Swaya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Kampuni ya
Uendelezaji Nishati ya Jotoardhi (TGDC) wakifuatilia uwasilishwaji wa
mada toka kwa Meneja Mkuu wa TGDC hivi karibuni mkoani Mbeya.
………………………………………………………………………………….
Habari Picha na Benedict Liwenga, Maelezo-Mbeya.
Mkoa wa Mbeya unasemekana kuwa
ni moja ya maeneo yaliyobarikiwa kuwa miongoni mwa maeneo ambayo Shirika
la Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) linatarajia kuanza shughuli
ya uchimbaji jotoardhi kutokana na tafiti za awali kuhusu nishati hiyo
kuanza katika mkoa huo.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja
Mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe wakati wa Kampeni ya Uelimishaji
kuhusu Jotoardhi kwa viongozi katika ngazi za Kata za Ilomba katika
Vijiji vya Ituha, Tonya pamoja na Kata nyingine ya Nanyala iliyoko Mbozi
Mkoani Mbeya.
Mhandisi Njombe amesema kuwa,
TGDC ina malengo ya kuzalisha zaidi ya megawati 200 kwa mkoa huo licha
ya mkoa huo kwa sasa kutumia megawati 40 jambo ambalo linaweza kupelekea
nishati hiyo itakayozalishwa kupeleka katika mikoa mingine ya jirani
kwani kiasi hiko cha umeme kitakuwa ni kikubwa.
Aidha, amewataka wakazi wa Mbeya
kuonyesha ushirikiano kati ya Serikali yao pamojana TGDC ili zoezi hilo
lenye manufaa kwao liweze kufikiwa kwa maendeleo ya mkoa na vijijini
ambako kuna changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme pia kutatua tatizo
la mgao wa umeme katika mkoa huo.
“Tuunge mkono jitihada hizi za
Serikali ili walau nishati hii izidi kuendelezwa na ituokoe dhidi ya
hali ya umeme isiyokuwa na uhakika kwani tukishakuwa na uelewa na
kuelimisha wananchi na kutoa ushirikiano, tutakaa mkao wa kula kutokana
na nishati hii”, alisema Njombe.
Kwa upande wake Mjiolojia
Mwandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Bwana Jacob Mayalla
ameeleza kuwa kutokana na juhudi za Serikali, tafiti za jotoardhi nchini
zilizanza miaka ya 1976 hadi mwaka 1978 zikiwa kama tafiti za awali
ambazo ziliweza kubainisha maeneo katika nchi ya Tanzania kwenye maeneo
yaliyopitiwa na Bonde la Ufa ambapo viashiria vya jotoardhi vipo.
“Kwa Mkoa wa Mbeya, tafiti za
jotoardhi zilifanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia
Tanzania”, alisema Mayalla.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa masuala
ya Kiufundi toka Kampuni ya TGDC, Bwana Taramaeli Mnjokava ameyataja
baadhi ya matumizi ya moja kwa moja ya jotoardhi nchini ikiwemo matumizi
ya kiutalii ambapo maji ya jotoardhi huwekwa kwenye mabwawa hivyo
huvutia watalii wa ndani na nje ya nchi kwa kuyaoga na kuyaangalia jambo
ambalo linaongeza pato la taifa.
Aliongeza kuwa, maji ya
jotoardhi hufaa kwa matumizi ya uzalishaji wa samaki kwani samaki
hupenda maji yenye hali ya uvuguvugu kuliko yenye baridi hasa kwa maeneo
yenye baridi kama mkoa wa Mbeya, hivyo pindi mabwawa ya samaki
yanapotengenezwa na kuwekewa maji ya jotoardhi yanasaidia kuzalisha
samaki kwa wingi jambo ambalo nalo litakuza pato kwa taifa na kwa eneo
husika ambalo uzalishaji unafanyika.
“Maji ya jotoardhi yanaweza
kutumika katika uzalishaji wa mboga mboga au maua kwa njia ya Vitalu
Nyumba kwa Kiingereza huitwa Green Houses lakini ni vitalu hutengenzwa
kwa plastiki au kioo, hivyo watu hutumia vitalu hivi jambo ambalo
linavutia sana soko la nje kwani huwa hawapendi mboga zilizopigwa dawa
wala maua yaliyopigwa dawa, niwahamasishe kujiandaa kwa kuupokea mradi
huu kwani utawanufaisha vyakutosha nyie wakazi wa Mbeya na taifa kwa
ujumla,” alisema Mnjokava.
Mnamo tarehe 19 Disemba, 2013
Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO)
ilisajiri kampuni ya kuendeleza nishati itokanayo na Jotoardhi, jina la
kampuni likiitwa “Tanzania Geothermal Development Company Limited
(TGDC).
Kampuni hii ilianzishwa kama
kampuni tanzu ya Shirika la TANESCO ambalo linamilikiwa na Serikali kwa
asilimia 100 na mnamo mwezi Julai 2014 TGDC ilianza kazi zake rasmi
ikipewa jukumu la kuharakisha uendelezaji wa nishati ya jotoardhi
nchini.
Post a Comment