Header Ads

Rais wa RT, Anthony Mtaka aula Shirikisho la Riadha la Dunia (IAAF)

Rais wa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) Lord Sebastian Coe (kushoto) akipeana mkono na Rais wa Shirikisho la riadha Tanzania (RT) Anthony Mtaka.

Na Dixon Busagaga.

SHIRIKISHO la mchezo wa Riadha Duniani (IAAF) limemteua Rais wa Shirikisho la Riadha nchini (RT) Anthony Mtaka kuwa miongoni mwa wajumbe wanaounda kundi la ushauri wa mikakati ya mawasiliano la shirikisho hilo.


Rais wa IAAAF ,Lord Sebastian Coe alitangaza uteuzi huo hivi karibuni ambapo wajumbe wengine ni Abrahamson Alan wa Marekani, Rodan Joe Junior ,Sierra  Calixto  ,,Karamarinov  Dobromir  kutoka  Bulgaria na Rochdi Souad  wa Ufaransa.


Akizungumza kuhusu uteuzi huo Mtaka ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Simiyu alisema amepokea uteuzi huo kwa furaha kutokana na kuwa ni nafasi ya juu katika sekta maarufu ya michezo katika ngazi ya kimataifa.


“Nimefurahishwa na uteuzi huu hasa ukizingatia nimeteuliwa nikiwa rais wa shirikisho la riadha mwenye umri mdogo kuliko wote kwa sasa takuwa na fursa ya kujifunza mambo mengi mazuri.”alisema Mtaka.


Alisema uteuzi huo ni faida kubwa kwa maendeleo ya michezo katika taifa letu, hasa kipindi hiki ambapo serikali ya awamu ya tano inapoandaa mkakati wa kuiweka sekta ya michezo kuwa sehemu kubwa ya ajira.


Mtaka alisema Tanzania itapata nafasi pana zaidi ya kuwakilishwa katika mikutano mikubwa ya mchezo wa riadha duniani (Decision Making) eneo ambalo linatoa fursa kubwa kwa maandalizi ya mashindano makubwa yajayo baada ya mashindano ya Olyimpiki yatakayofanyika katika jiji la Rio de Jeneiro mwaka huu.


“Taifa litarajie uwakilishi wenye tija, sababu mimi nimeteuliwa kati ya wajumbe nane  ambao kila mmoja wao anawakilisha eneo kubwa, hivyo kama nimepewa dhamana ya kuiwakilisha bara zima la Africa, kwa vyovyote nitaweka maslahi ya nchi yangu mbele bila kuathiri utendaji wa jukumu nililopewa.”alisema Mtaka.


“ Uteuzi wangu ni sifa kwa taifa zima, sifa ambayo itafufua mtazamo mwema ulioonyeshwa na wanariadha wakongwe walioiletea taifa sifa kama Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Gidamis Shahanga, Juma Ikangaa bila kumsahau Mzee John Stephen Akhwari aliyeshiriki Mexico City Games 1968.”aliongeza Mtaka.


Aidha Mtaka alisema uteuzi huo umeongeza hamasa ya kuwekeza maradufu katika kambi ya timu ya taifa ya riadha iliyopo katika hosteli ya Chuo cha misitu cha FITI kilichopo West Kilimanjaro wilayani Siha na Arusha.

No comments

Powered by Blogger.