Mama MARIA NYERERE atembelea Daraja la NYERERE Kigamboni, Apongeza Jitihada za Serikali na Watanzania
Na Mwandishi Maalum
Mke wa Rais wa
Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Maria Nyerere ametembelea Daraja
la Nyerere linalounganisha eneo la Kigambaoni na Kurasini Jijini Dar es salaam
na kuipongeza serikali na wananchi wote wa Tanzania kwa kufanikisha ujenzi wa
Daraja hilo kubwa na la kisasa kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.
Mama Maria Nyerere
aliyeongozana na Mwanae Mheshimiwa Makongoro Nyerere amesema kukamilika kwa
daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 254.12 kumekamilisha
mpango wa miaka mingi ulioanzishwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere aliyekuwa na nia ya kujenga daraja katika eneo hilo la mkondo
wa bahari lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti haikuwezekana.
Aidha, Mama Maria
Nyerere amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kuamua Daraja hilo liitwe Daraja
la Nyerere kwa heshimu ya Baba wa
Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na amebainisha kuwa uamuzi huo
utaviwezesha vizazi vijavyo kutambua juhudi zilizofanywa na mmewe katika ujenzi
wa nchi.
"Mimi
ninamshukuru sana Rais kwa maana ilikuwa lipewe jina lake, lakini yeye Mungu
akamjaalia akasema kwamba hapana tukumbuke tulikotoka, kwa hiyo najisikia
vizuri sana, na familia nayo inajisikia vizuri sana, lakini zaidi na watanzania
wanajisikia vizuri sana, kwa maana watakuwa wanaulizana Nyerere alikuwa ni
nani?" Amesisitiza Mama Maria Nyerere.
Daraja la Nyerere
lenye urefu wa meta 680, upana wa meta 32, njia sita za magari na barabara
unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5, lilifunguliwa na Rais wa awamu ya tano
Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 19 Aprili, 2016 na linakuwa kiunganishi muhimu
kati ya Kigamboni na katikati ya Jiji la Dar es salaam.
Post a Comment