Rais Dkt JOHN MAGUFULI amelitaka Jeshi la Polisi na Mawakili Kuwa Wazalendo
Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi nchini
na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujirekebisha kwa kutekeleza wajibu wao huku
wakitanguliza maslahi ya taifa.
Rais Magufuli
ametoa maagizo hayo leo tarehe 29 Aprili, 2016 wakati akifungua kikao cha kazi
cha Makamanda wa polisi wa mikoa, Mawakili wafawidhi wa serikali wa Mikoa na Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na
Vikosi, kinachofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Mikutano wa Dodoma
uliopo katika eneo la Tambukareli Mjini Dodoma.
Awali kabla ya
kutoa hotuba yake Rais Magufuli aliwapa nafasi Makamanda na Mawakili Wafawidhi
hao kutoa maoni yao juu ya changamoto zinazowakabili katika kutekeleza wajibu
wa kufanya upepelezi na kuendesha mashitaka, hususani kujua sababu za
kuchelewesha kesi za makosa ya jinai, ambapo wamedai ufinyu wa bajeti ndio
sababu kubwa ya kucheleweshwa kwa kesi za hizo.
Baadhi
ya Makamanda wa polisi wa Mikoa mbalimbali wakipiga makofi wakati Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa
akiwahutubia.
|
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kufungua kikao kazi hicho. |
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na
Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Mohamed Mpinga.
|
Kufuatia kutajwa
kwa changamoto hiyo Rais Magufuli ameahidi kuhakikisha anawatafutia fedha kwa
ajili ya kukabiliana nazo, lakini ametaka fedha zitakazotafutwa zitumike vizuri
kwa kuwa taarifa zinaonesha Jeshi la Polisi limekuwa likihusishwa na matumizi
mabaya ya fedha hali inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji
wake wa kazi.
Ametolea mfano wa
taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kununulia vifaa
na sare za askari, ama mikataba yenye mashaka inayotiwa saini kati ya Polisi na
wawekezaji kuwa ni baadhi ya mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa
jeshi hilo.
"Oysterbay
pale ni eneo ambalo ni very prime, kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba
mnayoijua nyinyi, akapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo
yanafaa. Palikuwa na ubaya gani eneo la Oysterbay likawa na hati, mkaitumia
hiyo hati kwenda kukopa benki na kujenga nyumba hata za ghorofa 20 pale,
mkaweka investment na Polisi wenu
wakakaa pale. Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa uwazi nitajisikia
vibaya nikimaliza mkutano huu,
nataka muelewe na muelewe ukweli direction
ninayoitaka mimi" Amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais
Magufuli ameitaka Ofisi ya mwendesha Mashitaka wa Serikali kujipanga kufanya
kazi kwa ufanisi na ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya serikali
kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya kuwa na wanasheria mahiri.
"Niwaombe
mawakili na polisi wanaohusika na upelelezi mtangulize maslai ya nchi mbele,
kwa sababu kumekuwa na usemi kwa baadhi ya wapelelezi na mawakili wachache,
nasema wachache, panapokuwa na kesi inayohusiana na pesa pesa, wana misemo yao
wanasema dili limepatikana, na saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani
wana-collude Mawakili wa serikali na mawakili wanaomtetea mhalifu, na wanapo-collude siku zote serikali
inashindwa. Unapoona hali hiyo ya kila siku serikali inashindwa, halafu siku
hiyo unataka serikali ikuwezeshe, kwa vyovyote serikali inapata kigugumizi"
amesisitiza Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli pia
amelitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na kashfa ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi
yake, ikiwemo maafisa wa Polisi kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na
kuazimisha silaha kwa wahalifu wa ujambazi.
Hata hivyo Rais
Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kwa kazi kubwa wanayoifanya na
ametaka apelekewe mpango wa mahitaji yao ili atafute namna ya kuimarisha vyombo
hivyo.
Post a Comment