Rais Mstaafu Jakaya
Kikwete katika mahojiano na Ndugu Amarildo Da Conceiacao kutoka Taasisi ya DKt Agostine Neto, Mpigania Uhuru na Rais wa Kwanza wa Angola jijini Dar es Salaam
jana.
Na Mwandishi Maalum
Rais
Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ametembelewa na ujumbe kutoka Taasisi ya Dkt.
Agostinho Neto ya Angola jana jijini Dar es Salaam.
Ujumbe wa Taasisi hiyo unaoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Amarildo Da
Conceicao uko nchini kwa lengo la kufanya mahojiano na viongozi wa Tanzania kwa
lengo la kuhifadhi historia ya mpigania uhuru na muasisi wa Taifa la Angola
Dkt. Agostinho Neto.
Akimuelezea Dkt. Agostinho Neto, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete amemzungumzia
mpigania uhuru huyo kuwa mtu mwenye kuzungumza kwa sauti ya upole lakini
kiongozi makini, shupavu na mwenye uwezo mkubwa wa kifalsafa na kifikra. Dkt.
Kikwete amesema anakumbuka akiwa kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, walimualika Dkt. Neto kuja kuzungumza na wanafunzi katika Darasa
la Itikadi alipozuru nchini mwaka 1974.
Mpigania uhuru huyo aliyembatana na mkewe mwenye asili ya kireno aliulizwa
swali na mwanafunzi mmoja, 'iweje yeye ni mpigania uhuru dhidi ya watu weupe
ilihali ameoa mwanamke mweupe?'. Katika jibu lake, Dkt. Neto alisema,
'mapambano hayana rangi, hatupambani na watu weupe tunapambana na ukoloni, mtu
mweupe anaweza kuungana nasi katika mapambano yetu hali kdhalika wapo wenzetu
weusi wanaoungana na kusaidia wakolini dhidi yetu'.
Rais
Mstaafu amewapongeza Taasisi ya Agostinho Neto kwa jitihada inazochukua za
kuhifadhi historia ya mpigania uhuru na muasisi wa Taifa la Angola.
Amewakumbusha umuhimu wa kuhakikisha
kuwa historia hiyo inarithishwa kwa kizazi baada ya kizazi ili watambue
tulipotoka, tulipo na tunapotakiwa kwenda.
Ujumbe wa Taasisi ya Neto pia umefanya mahojiano kama hayo na Mama Maria
Nyerere, Mke wa Baba wa Taifa, Mheshimiwa Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu
Mstaafu na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Nchi za Kiafrika (OAU) na viongozi
na watanzania mashuhuri ambao walishiriki kwa namna moja au nyingine katika
harakati za uhuru wa Angola.
Imetolewa na Ofisi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,
Dar es Salaam
2Aprili, 2016
|
Post a Comment