Mafunzo ya Wasimamizi wa Uchaguzi Mkoa wa Dar es Salaam yafanyika
Na Aron Msigwa- MAELEZO
Mkuu
wa mkoa wa Dar es slaam Said Mecki Sadiki amewataka Waratibu wa
Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi na viongozi wa vyama vya Siasa katika
mkoa huo kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao kwa ushirikiano ili
kuwawezesha wananchi kupiga kura kwa amani na utulivu wakati wa uchaguzi
mkuu wa Rais ,Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Akifungua
mafunzo ya siku mbili ya waratibu wa Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi,
Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi na Maafisa uchaguzi leo jijini Dar es
salaam Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa Dar es salaam ni miongoni mwa
maeneo yenye wapiga kura wengi hivyo mkoa kwa kushirikiana na Tume ya
uchaguzi umejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wote waliojiandikisha
wanapiga kura kwa amani na utulivu Siku ya uchaguzi Oktoba 25 mwaka huu.
Amesema
Wakurugenzi wa Halmashauri wa mkoa huo ambao ndiyo wasimamizi wa
uchaguzi katika wilaya wanalo jukumu la kuwaita na kuwaelimisha viongozi
wa vyama vya siasa juu ya taratibu na kanuni za kufuata wakati wa
uchaguzi mkuu ili wajenge mazingira rafiki ya kufanya kazi kwa
ushirikiano.
Aidha, amewasisitiza wasimamizi
hao kutojihusisha kwa namna yoyote ile na kampeni za siasa wakati wa
kutekeleza majukumu yao kwani kufanya hivyo watakuwa wanahujumu ufanisi
wa uchaguzi mkuu katika mkoa wa Dar es salaam.
Ili
kudumisha amani na utulivu vituoni amewataka kufanya kazi zao kwa
umakini mkubwa kwa kuwa suala la amani vituoni litakuwa mikononi mwao
wakati wa kipindi chote cha upigaji wa kura Oktoba 25 mwaka huu.
"Simamieni
kanuni, sheria na taratibu, msionyeshe upendeleo wowote wala kufanya
kampeni ya aina yoyote ile ndani ya vituo vya kupigia kura, jambo hilo
halikubaliki hata kidogo,mfanyeni kazi mliyotumwa ili msiwe sehemu ya
tatizo katika nchi hii" Amesisitiza Sadiki.
Ametoa
wito kwa wananchi kuendelea kutunza kadi zao za kupigia kura ili waweze
kuzitumia siku ya uchaguzi na kuvionya vikundi, watu au vyama
vinavyojaribu kuwarubuni wananchi kwa kununua kadi zao za kupigia kura
kuacha tabia hiyo.
" Watu wanaofanya hivi
wanafanya unyang'anyi, nawataka waache tabia hii kwani haina tija kwa
mamaendeleo ya taifa letu,ukichukua au kuiba kadi ya mtu unamnyima haki
ya kupiga kura muhusika na huo sio uungwana" Amesisitiza.
Ametoa
wito wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kudumisha amani wakati wa
upigaji wa kura na kuwataka wananchi wote waliopanga kufanya vurugu
wakati wa uchaguzi kuacha
"Sisi kama Serikali
hatuvumilia aina yoyote ya uvunjifu wa amani, tutaimarisha ulinzi yapo
maeneo korofi ambayo yamekuwa na vitendo vya uvunjifu wa amani
tunayajua, tunawahakikishia wananchi watapiga kura kwa amani na kurudi
makwao wakiwa salama"
Kuhusu waangalizi wa
Kimataifa waliowasili nchini ambao baadhi yao watafanya kazi jijini Dar
es salam amesema watafanya kazi zao kwa mujibu wa taratibu na kanuni
walizopewa na Tume na kuongeza kuwa kazi yao itakua ni kuangalia kama
tumnazingatia na kufuata sheria tulizojiwekea na si kuingilia shughuli
za wasimamizi wa zoezi la upigaji wa kura.
"Suala
la kusimamia zoezi la upigaji wa kura ni letu wenyewe, msiwaruhusu
waanze kuwapa taratibu za upigaji wa kura wa nchi walizotoka wala kutoa
maamuzi yoyote, kazi yao itakua ni kuangalia mwenendo wa uchaguzi wetu
na si vinginevyo" amesisitiza.
Aidha, amevitaka
vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinawapeleka mawakala wao mapema
katika vituo vya kupigia kura kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji wa
kura ili kuondoa manung'uniko yanayoweza kujitokeza.
Kwa
upande wake Bi. Clesensia Mayala ambaye ni Kaimu Mkuu wa Sehemu, Kanda
ya Kusini Tume ya Taifa ya Uchaguzi amesema lengo la mafunzo hayo ni
kuwakumbusha wasimamizi na Maafisa uchaguzi kuzingatia na kufuata
taratibu zilizotolewa na Tume ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Amesema
katika mafunzo hayo washiriki hao watajadili masuala mbalimbali ikiwemo
wajibu na majukumu ya waratibu na wasimamizi wa uchaguzi,majukumu ya
makarani waongozaji wa vituo vya kupigia kura ,kuangalia fomu
zitakazotumika wakati wa upigaji kura,taratibu za upigaji kura, Fomu
zitakazotumika wakati wa kuhesabukura, kujumlisha na kutangaza matokeo
ya Urais,Wabunge na Madiwani.
Amefafanua kuwa
wasimamizi wote wa uchaguzi watakua na jukumu la kuhakikisha kuwa vituo
vyote ya uchaguzi vinafunguliwa kwa wakati na kufungwa kwa kuzingatia
muda uliopangwa ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanatimiza wajibu wao
wa kikatiba.
Kwa upande wake Msimamizi wa
Uchaguzi Wilaya ya Temeke Bw. Photidas Kagimbo amesema uchaguzi mkuu
katika eneo analolisimamia utafanyika kwa uhuru na usalama na kuongeza
kuwa wamejipanga vyema kuwahudumia wananchi wote waliojiandikisha ambao
watajitokeza kupiga kura siku hiyo.
Amesema
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kupeleka vifaa mbalimbali katika
maeneo mbalimbali ili kuwawezesha wananchi kupiga kura Oktoba 25 na
kufafanua kuwa kazi inayoendelea sasa ni utoaji wa elimu ya mpiga kura
kwa wananchi.
Kuhusu suala la uhakiki wa
taarifa za wananchi katika daftari la kudumu la Wapiga kura kwa wananchi
walioshindwa kuhakiki kutokana na sababu mbalimbali amesema liko
mikononi mwa Tume ya Taifa ya uchaguzi na kwamba wao wanasubiri
maelekezo ya Tume hiyo na daftari kamili litakalokuwa na orodha ya
wapiga kura wote litakalopelekwa kwenye vituo vya kupigia kura kabla ya
tarehe ya uchaguzi ili kutoa fursa kwa vyama vya siasa na wananchi
kupitia majina yote.
Post a Comment