Serikali yasisitiza Matumizi ya TEHAMA
Na Aron Msigwa –Maelezo
Serikali imesema kuwa itaendelea kuboresha
miundombinu yake ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kote nchini
ili kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za Serikali kwa uwazi mahali walipo kupitia
mtandao.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.HAB Mkwizu wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maendeleo ya Serikali Mtandao na
malengo ya baadaye ya uimarishaji wa matumizi ya TEHAMA katika shughuli za
Serikali.
Amesema ili kuimarisha uwazi na upatikanaji wa
Takwimu huria,Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya TEHAMA kwa lengo la
kuwawezesha wananchi kupata huduma zinazotolewa na Wizara na Taasisi za
Serikali kupitia simu zao za mkononi mahali walipo.
Ameeleza kuwa ili kulinda na kuthamini mafanikio
yaliyopatikana nchini Tanzania Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
kupitia Wakala ya Serikali Mtandao(e Government Agency) imeandaa Mkutano Mkuu
wa mwaka wa wataalamu wa TEHAMA na Watendaji Wakuu wa Serikali utakaofanyika
jijini Arusha kuanzia Agosti 17 hadi 20 mwaka huu.
Bw. Mkwizu amesema kuwa Mkutano huo utafunguliwa na Katibu Mkuu kiongozi
Balozi Ombeni Sefue chini ya kauli mbiu isemayo Kaulimbiu ya
Mkutano huo ni Uwezeshaji wa Wananchi kupitia TEHAMA.
Amesema kuwa washiriki
zaidi ya 500 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali zinazotoa huduma kwa umma
watapata fursa ya kujadili masuala
mbalimbali ya ushirikiano katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao nchini
Tanzania, Kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo ili kuleta maendeleo
ya kiuchumi na kijamii.
Amebainisha kuwa kupitia mkutano huo washiriki
watazungumzia namna bora ya uimarishaji wa utoaji wa huduma kwa umma kupitia
ushirikiano wa maarifa na ukuzaji wa uhusiano wa
kikazi.
Aidha, wataalam wa TEHAMA wa Tanzania watapata fursa
ya kujifunza kutoka. Kwa wataalam wengine wanaohusika
na Serikali Mtandao kutoka nchi zinazofanya vizuri katika eneo la Serikali
mtandao zikiwemo India na Singapore.
Bw.Mkwizu ameeleza kuwa wakati wa
mkutano huo mada mbalimbali zitajadiliwa zikijikita katika usimamizi wa Serikali Mtandao nchini
Tanzania, Hali ya miundombinu ya
Serikali mtandao na Utekelezaji wa Mpango wa Uendeshaji wa Serikali kwa uwazi .
Mada nyingine zitahusu uimarishaji
wa uwazi na Mfumo wa Takwimu huria nchini Tanzania na uimarishaji wa huduma za
Serikali kwa wananchi kupitia simu za mkononi na mifumo inayotumika kutoa huduma kwa
wananchi.
Post a Comment