POLISI ; Wagombea Urais Marufuku Kuambatana na Wapambe
Jeshi la Polisi nchini
limesitisha maandamano ya wafuasi wa vyama vya siasa wakati wa kuchukua
,kutafuta wadhamini, na kurejesha fomu za kugombea nafasi ya Urais
katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam Naibu Inspekta Jenerali wa jeshi la
Polisi Abdulrahman Kaniki amesema kuwa jeshi limechukua hatua hiyo
kutokana na ukiaukwaji wa sheria za usalama barabarani uliojitokeza
wakati wagombea wa vyama vya CHADEMA na CCM walipochukua fomu za
kugombea Urais makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Kwa sababu za kiusalama Jeshi
la Polisi linasitisha maandamano ya aina yoyote wakati wote wa zoezi la
kuchukua fomu, kutafuta wadhamini mikoani pamoja na zoezi la kurejesha
fomu “ alisema Kaniki.
Aidha aliongeza kuwa jeshi la
Polisi nchini linafanya utaratibu wa kuwakutanisha wadau wote wa siasa
ikiwemo viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi Mkuu
ili kuona namna bora ya kufanya uchaguzi katika hali ya amani na
utulivu.
“Jeshi la Polisi halitasita
kumchukulia hatua za kisheria mgombea, kiongozi, mfuasi au chama
chochote cha siasa kitakachokiuka agizo hili,” alisema.
Hatua hiyo ya jeshi la Polisi
nchini inatokana na baadhi ya wagombea wa nafasi za Urais kufuatana na
kundi kubwa la wanachama, na wapambe wao wakati wa kuchukua fomu za
kuomba kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ofisi za
Tume ya Taifa ya Uchaguzi hivi karibuni na kuatarisha usalama ikiwemo
kufungwa kwa barabara na kusababisha baadhi ya shughuli za kijamii
kusimama.
Post a Comment