Pato la Taifa la Robo ya Kwanza ya Mwaka 2015, Limefikia Shilingi Trilioni 21.9
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Morrice Oyuke (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu pato la taifa robo ya kwanza ya mwaka kuanzia Januari hadi machi 2015. Kushoto ni Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa, Daniel Masolwa.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Morrice Oyuke (kulia), akisisitiza jambo katika mkutano huo.
Wapiga picha za habari na wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Na: Veronica Kazimoto
Matokeo ya takwimu za Pato
la Taifa kwa robo mwaka ya kwanza yaani kuanzia mwezi Januari – Machi, 2015 yameonyesha
kuwa thamani ya Pato la Taifa imekua na kufikia shilingi trilioni 21.9 ikilinganishwa
na shilingi trilioni 18.6 ya robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2014.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Morrice Oyuke amesema takwimu hizo zimetayarishwa
kwa kuzingatia marekebisho ya Takwimu za Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2007.
“Pato la Taifa kwa bei za mwaka
2007 katika kipindi cha robo mwaka ya kwanza linaonyesha kuwa na jumla ya
thamani ya shilingi trilioni 10.6 kwa mwaka 2015 ikilinganishwa na shilingi trilioni
9.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2014”, amefafanua Oyuke.
Oyuke amesema kuwa, Pato
hili la Taifa limeongezeka kwa kasi ya asilimia 6.5 katika kipindi cha robo ya
kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 8.6 katika kipindi kama
hicho mwaka 2014.
Aidha, Oyuke amesisitiza
kuwa utayarishaji wa takwimu za Pato la Taifa hujumuisha shughuli zote za
kiuchumi na hivyo hutumika katika kutathmini, kupanga mipango na kutayarisha
sera za kiuchumi.
Baadhi ya shughuli hizo za
uchumi ni kilimo na mifugo ambazo zilikua kwa kasi ya asilimia 2.6 katika
kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa
asilimia 3.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Shughuli
za Uvuvi ziliongezeka kwa asilimia 0.9 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa
na asilimia 2.3 kipindi kama hicho mwaka 2014. Ukuaji huu ulitokana na jitihada
za Serikali kuwasaidia wakulima kwa kutoa ruzuku na maelekezo ya Ma-ofisa Ugani
kwa wakulima kama vile kuchagua mbegu bora yaliyosaidia kuongeza uzalishaji.
Shughuli za Uchimbaji Madini,
Mawe na Kokoto ziliongezeka kwa kasi ya asilimia 0.6 katika kipindi cha robo ya
kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 19.7 katika
kipindi kama hicho mwaka 2014.
Shughuli
za Uzalishaji bidhaa Viwandani zilikua kwa
kasi ya asilimia 5.7 katika
kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 8.2
kipindi kama hicho mwaka mwaka 2014. Kasi
ya ukuaji ilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa za vyakula, vinywaji,
tumbaku, nguo, simenti na bidhaa za kemikali na madawa.
Shughuli
nyingine ni pamoja na Uzalishaji nishati ya umeme na maji ambazo zilikua kwa
kasi ya asilimia 10.7 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015
ikilinganishwa na kasi ya asilimia 10.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Kuongezeka kwa ukuaji wa nishati ya umeme kulitokana na kuongezeka kwa umeme
uliozalishwa kutoka kwenye mitambo inayotumia, maji, mafuta na gesi asilia.
Shughuli
za Fedha na Bima katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ziliongezeka
kwa asilimia 9.1 ikilinganishwa na asilimia 11.2 kipindi kama hicho mwaka 2014.
Shughuli
za Ujenzi (ambazo zinajumuisha
ujenzi wa nyumba za makazi na zisizo za makazi; barabara na madaraja; na
shughuli nyingine za uhandisi) katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015
ziliongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa
na asilimia 21.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu ina jukumu la kutayarisha na kusambaza takwimu rasmi nchini
ikiwa ni pamoja na takwimu za Pato la Taifa kwa robo Mwaka ambazo hupimwa kwa
kuangalia thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa nchini katika vipindi vya
miezi mitatu mitatu ambavyo ni Januari – Machi, Aprili – Juni, Julai – Septemba na Oktoba - Desemba.
Post a Comment