Header Ads

MUWANIA UBUNGE JIMBO LA KAWE, WAKILI ELIAS NAWERA, AELEZEA KUHUSISHWA NA RUSHWA

  Mgombea nafasi ya kuwania ubunge Jimbo la Kawe, Wakili Elias Nawera (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi.
 Mgombea nafasi ya kuwania ubunge Jimbo la Kawe, Wakili Elias Nawera (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu kumpa ushirikiano mgombea wa nafasi hiyo aliyeshinda kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo hilo na kukamatwa kwake na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa madai ya kutoa rushwa.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.

Na Dotto Mwaibale

MGOMBEA nafasi ya kuwania ubunge Jimbo la Kawe, Wakili Elias Nawera amesema atampa ushirikiano mgombea wa nafasi hiyo aliyeshinda kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhakikisha CCM inapata ushindi.

Nawera aliyasema hayo jijini Dar es Salaam leo asubuhi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato wa kura za maoni katika jimbo hilo na kuhusishwa na kukamatwa kwake na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa madai ya kutoa rushwa.

"Nampongeza mwenzangu aliyeongoza kura za maoni katika jimbo la Kawe na ninaahidi kushirikiana na mgombea mwenzangu atakaye teuliwa na vikao vya uteuzi vya CCM kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu na kuwa ushindi wa kishindo kwa CCM kuanzia udiwani, ubunge na urais".  alisema Nawera.

Akizungumzia kuhusu mchakato huo na kuhusishwa na rushwa aliilalamikia Takukuru kwa kumuhusisha na tukio hilo kuwa walikuwa na nia ya kumsaidia mmoja wa wagombea nafasi hiyo na yeye kumpunguza nguvu kisiasa.

Nawera alisema licha ya kutoa taarifa za vitendo vya rushwa katika mchakato huo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa lakini katika mazingira ambayo hakuyategemea amebambikiwa tuhuma hizo ambazo hakuwa nazo.

Aliongeza kuwa wakati wa ukamatwaji wake hawakumjulisha kuwa yupo chini ya ulinzi, pia hawakujitambulisha na wala hawakumuambia anatuhumiwa kwa kosa gani na bila kumpa nafasi ya kuwasiliana na ndugu zake au mwanasheria na kumpeleka kituo cha polisi Magomeni.

Nawera alisema si jambo zuri kwa vyombo vya dola kumkamata mwananchi na kumuhusisha na tuhuma mbalimbali hiyo si sahihi na ni matumizi yasiyofaa ya rasilimali za nchi na matumizi mabaya ya madaraka.

Muwania ubunge huyo Julai 30, 2015 saa mbili usiku alikamatwa na maofisa wa Takukuru kwa kuhusishwa na rushwa na baada ya mahojiano alisweka rumande kwa masaa 10 na kuachiwa kwa kujidhamini mwenyewe. 

No comments

Powered by Blogger.