Jamii yashauriwa Kushiriki Mazoezi ya Viungo vya Mwili ili Kujenga Afya Zao
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akishiriki matika kufanya mazoezi ya kunyoosha viungo katika Viwanja vya Mnazi mmoja Wete. |
Baadhi ya vikundi vya mazoezi vikishiriki matembezi hayo ya mazoezi. |
Vijana wa Brasband wakisherehesha matembezi hayo ya mazoezi. |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wanavikundi wa mazoezi katika Viwanja vya Mnazi mmoja Wete. |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi zawadi ya vifaa vya mazoezi kwa mmoja kati ya wanamazoezi hao. |
Na:
Hassan Hamad (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameuthibitishia ulimwengu kuwa
yuko katika afya njema, baada ya kuongoza matembezi ya mazoezi kwa zaidi ya
kilomita sita.
Matembezi hayo yaliyoanzia
eneo la Tungamaa hadi viwanja vya Mnazi mmoja Wilaya ya Wete, yamevishirikisha
vikundi kadhaa vya mazoezi kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza baada ya
matembezi hayo, Maalim Seif amesema yuko vizuri na anaweza kutembea kwa mazoezi
mara mbili zaidi ya neo hilo alilotembea.
Ametoa wito kwa
wananchi wa Zanzibar kushiriki katika mazoezi ili kuimarisha afya zao, kwani
mazoezi ni sehemu ya tiba mbadala kwa maradhi mbali mbali yakiwemo sukuri,
presha na maumivu ya viungo.
Amefahamisha kuwa
wananchi wengi waliojiunga na vikundi vya mazoezi wakiwa na matatizo hayo
tayari wamepata nafuu, na sasa hawapendi tena kuacha kufanya mazoezi kwani
kufanya hivyo ni kukaribisha maradhi yasiyokuwa na ulazima.
Aidha Maalim Seif
ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuandaa programu za
kuyatangaza mazoezi nchini, ili wananchi waweze kushajiika zaidi kufanya
mazoezi.
Amesema nchi nyingi duniani
ikiwemo uchina, zimekuwa zikishajiisha mazoezi kwa watu wa rika zote wakiwemo
vikongwe, hali inayosaidia kulinda afya za wananchi hao na kupunguza gharama za
matibabu.
Katika kuunga mkono
mazoezi hayo, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa zawadi ya vifaa
vya michezo kwa baadhi ya vikundi vya mazoezi katika Mkoa huo, na kuahidi
kuchangia vifaa zaidi kwa makundi mengine yaliyobakia.
Nae Waziri wa Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk, amempongeza Maalim Seif kwa
ujasiri wake wa kushajiisha wananchi kufanya mazoezi, hali inayotoa mwamko kwa
wananchi wengi kuanza kufanya mazoezi.
Amesema baada ya
Makamu wa Kwanza wa Rais kuzindua vikundi vya mazoezi katika Jimbo la Gando
mwezi April mwaka huu, kisiwa cha Pemba kilikuwa na vikundi 30 vya mazoezi,
lakini ndani ya kipindi cha miezi minne vimeongezeka kufikia vikundi 60.
Ameeleza kuwa Wizara
ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo itaendelea kushirikiana na vikundi vya
mazoezi ili kuona kuwa hali ya mazoezi inakwenda vizuri, na kuwawezesha
wananchi wengi zaidi kuweza kushiriki.
Mapema akisoma risala
ya vikundi hivyo vya mazoezi nd. Omar Dadi amesema wamefarajika baada ya Makamu
wa Kwanza wa Rais kutekeleza ahadi yake na kushiriki katika matembezi hayo ya
mazoezi.
Amesema utaratibu wa
kufanya mazoezi umewasaidia sana wananchi wa Kisiwa cha Pemba kiafya, na
kuwashauri wananchi wengine kuanza kufanya mazoezi bila kujali shughuli na umri
walionao.
Post a Comment