Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe akifafanua jambo kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Viongozi wa juu na kuwatumikia wananchi kwa kupunguza changamoto zilizo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, mara baada ya Waziri wa Nchi kushoto kwake George Simbachawene kutoa hotuba yake kwa Baraza la Wafanyakazi lililofanyika katika Ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma. .........................................
Na Augusta Njoji, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), George Simbachawene amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, sambamba na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwenye utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza katika kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika mjini Dodoma, Simbachawene amesema watumishi hao wanatakiwa kuwa na utendaji unaojali matokeo na kuepuka utendaji wa mazoea.
Amesema wanatakiwa kuzingatia nidhamu na utendaji wa Watumishi wa Umma,na watambue maadili ni nguzo muhimu ya kuepuka vitendo vya ubadhilifu na rushwa mahali pa kazi.
Hata hivyo, amesema kwasasa inafanya uchunguzi wa tuhuma za rushwa kwenye ofisi hiyo zinazotokana na uhamisho, upangaji wa walimu na michakato ya teuzi mbalimbali.
Waziri huyo amesema kumekuwa na tuhuma kwa baadhi ya watumishi kujihusisha na vitendo vya rushwa na kwamba watumishi watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Sambamba na hilo, ametaka kila Idara na kitengo kuhakikisha kuwa zinapunguza matumizi yasiyo ya lazima ili kuelekeza rasilimali fedha katika kutekeleza majukumu ya msingi ambayo yataleta tija kwa Taifa.
Simbachawene amewaambia wafanyakazi hao kuwa serikali itaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.
|
Post a Comment