Vyuo Vikuu Waaswa Kuepuka Migomo na Maandamano yasiyo na Tija Kwa Taifa
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda (kushoto) akizungumza na
Viongozi na watendaji wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) mara
baada ya kuwasili chuoni hapo kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano la 3
lililowakutanisha wahitimu wa chuo hicho mwaka huu, wanataaluma waliopo na wale
waliowahi kusoma katika chuo hicho (CBE Alumni Association) na wadau mbalimbali
jijini Dar es salaam.
Mwanafunzi wa
mwaka wa Pili katika Fani ya Utawala katika Biashara Vaileth Monyo (kulia) akitoa
ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali kuhusu fani hiyo kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Kipolisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda (kushoto) na Mkuu wa Chuo cha CBE Prof.
Emanuel Mjema (katikati) walipotembelea mabanda ya maonesho ya wanafunzi hao.
Wanafunzi wa
CBE, Adam Luhalala (kushoto) na Petro Nchimbi wakifanya ukaguzi wa Mashine ya
kutengeneza vipuri mbalimbali vinavyotumika kwenye mashine za viwandani na
Magari ndani ya Karakana ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Dar es
salaam.
Wahitimu wa
chuo CBE mwaka huu, wanataaluma waliopo na wale waliowahi kusoma katika chuo
hicho (CBE Alumni Association) na wadau mbalimbali waliohudhuria kongamano la 3
la chuo hicho jijini Dar es salaam.
Mwanafunzi wa
Mwaka wa 2 katika fani ya Vipimo Mathew Kaizilege akitoa ufafanuzi kuhusu
mashine ya kuchonga vipuri kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Jangwani walioitembelea
Karakana ya Vipimo ya CBE jijini Dar es salaam.
Na Mwandishi Wetu – Dar es
salaam.
Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu
ya juu kote nchini wametakiwa kutumia muda mwingi kujisomea na kuepuka
kujiingiza kwenye vitendo vya vurugu , migomo na maandamano yasiyo na tija kwa
taifa ambayo yamekuwa yakiwapunguzia ufanisi katika masomo yao.
Wito huo umetolewa na
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda wakati
akizungumza na Jumuiya ya wanataaluma wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es
salaam (CBE) kwenye kongamano la 3 lililowakutanisha wahitimu wa chuo hicho
mwaka huu, wanataaluma waliopo na wale
waliowahi kusoma katika chuo hicho (CBE Alumni Association) na wadau mbalimbali
jijini Dar es salaam.
Akiwa mgeni rasmi katika
kongamano hilo na mmoja wa wahitimu wa siku nyingi wa chuo hicho Kamanda Suzan
Kaganda amesema wanafunzi wa vyuo vya Elimu ya juu wanapaswa kutambua kuwa
elimu wanayoipata katika vyuo hivyo sio kwa ajili ya manufaa yao binafsi bali
ni kwa manufaa ya taifa zima hivyo wanatakiwa kuwa makini na kuwa mfano wa
kuigwa katika jamii.
“Naomba nisisitize kuwa
elimu mliyoipata na mnayoendelea kuipata chuoni hapa sio kwa ajili ya manufaa
yenu binafsi bali ni kwa ajili ya manufaa ya taifa, wakati mwingine mnapoteza
muda mwingi pindi mnapojiingiza kwenye migomo na maandamano barabarani
kushindana na Serikali, muda ambao mgeutumia kujisomea ninyi wenyewe”
Amesisitiza Kamanda Suzan.
Amewataka wahitimu na
wanafunzi wa chuo hicho kutumia elimu na ujuzi walioupata kusaidia katika
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali ya awamu ya tano kwa kuhakikisha
wanazitumia vizuri fursa za ajira zilizopo kujiajiri na kuajiri wengine.
“Taifa letu linazo fursa
nyingi, kinachotakiwa ni wazawa kuazisha makampuni yatakayoweza kuzalisha
bidhaa mbalimbali ambazo zitauzwa duniani na hatimaye kukuza uchumi wan chi
yetu” Amesisitiza.
Aidha, amekipongeza chuo
cha CBE kwa kupiga hatua na kupata mafanikio makubwa katika utoaji wa elimu
tangu kuanzishwa kwake miaka 51 iliyopita kwa kuwa maendeleo makubwa kwa taifa
lolote hayawezi kupatikana bila kuwaelimisha wake katika biashara na
Ujasiriamali elimu inayotafsiri uchumi wa viwanda pia.
“Nachukua fursa hii
kuupongeza uongozi wa CBE kwa kuongeza matawi ya chuo katika mikoa ya Dodoma,
Mwanza na Mbeya pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka
pamoja na fani katika ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada, Shahada za Uzamili
na Uzamivu” Amesema Suzan Kaganda.
Kwa upande wake Mkuu wa
Chuo cha CBE, Prof. Emanuel Mjema akizungumza wakati wa kongamano hilo amesema
kuwa chuo anachokiongoza kimeendedelea kupata sifa ya kuwa chuo bora ndani na
nje ya nchi kwa kuwa kimewatoa viongozi mahiri ambao waliotoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Ameeleza kuwa CBE
kilianzishwa mwaka 1965 kikiwa na wanafunzi 20 tu ili hali sasa kina wanafunzi
zaidi ya 11,000 huku fani za elimu zikiongezeka kutoka ngazi ya cheti hadi shahada za Uzamili na
masomo ya Uzamivu ambayo yanatolewa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha
Mashariki cha Finland.
“ Chuo chetu kimepiga hatua
kubwa kimaendeleo toka kilipoanzishwa mwaka 1965, kimepata mabadiliko makubwa
tumekuwa kitaaluma, kimachapisho na pia kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo fursa
za biashara wakati huu ambao Serikali inahamia mkoani Dodoma” Amesisitiza.
Ameongeza kuwa chuo hicho
kitaendelea kusimamia weledi katika utoaji wa elimu hapa nchini ili kiendelee
kutoa vijana wenye weledi na uwezo wa kutekeleza majukumu mbalimbali kulingana
na fani walizosomea.
“Chuo chetu tunasisitiza
ubora wa elimu, tunafanya mchujo kwa kila mwaka ili kudhibiti ubora wa elimu
yetu wale wasiofikia viwango kwa kila mwaka tunawaacha warudishwe nyuma sio
kila anayeingia hapa lazima ahitimu masomo yake wale wasiokidhi viwango na
kuendana na kasi ya masomo chuoni hapa wanajiondoa wenyewe” Amesisitiza Prof.
Mjema.
Katika hatua nyingine Prof.
Mjema amebainisha kuwa Novemba 12 Chuo hicho kitaadhimisha mahafali ya 51 tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1965.
Post a Comment