Geti la kuingilia katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani iliyopo katika Wilaya ya Muheza na Korogwe Mkoani Tanga.
Kinyonga aina ya pembe tatu (three hornes chameleon) ambao hupatikana katika hifadhi ya Mazingira Asilia Amani tu.
Moja ya vyura aina ya Usumbara (Leptopelis vermiculatus) ambao wanaopatikana katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani pekee.
Sehemu ya maporomoko
ya maji katika hifadhi ya Msitu wa asili ya amani iliyopo Wilayani Muheza
Mkoani Tanga ambayo imekuwa kivutio kwa watalii wanaotembelea eneo hilo.
Moja ya vyanzo vya maji katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani.
Moja ya aina ya vipepeo "Colourful moth (Utetheisa pulchella)" wanaopatikana katika Hifadhi ya Mazingira Amani pekee.
Kituo cha Taarifa katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani. Nyumba hii ilitumika na Kingozi wa Kituo cha Treni cha Mjerumani miaka 1904.
Na Hamza Temba - WMU
Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani ndiyo hifadhi kongwe kuliko hifadhi asilia zote nchini, Hifadhi hii ilitangazwa rasmi kwenye gazeti la Serikali mwaka 1997. Hifadhi hii ipo katika Wilaya za Muheza na Korogwe umbali wa kilomita 64 kutoka Jijini Tanga.
Amani yenye ukubwa wa hekta 8,380 ni moja kati ya maeneo ya mfano yaliyohifadhiwa vizuri nchini kwa kutumia mfumo wa Uhifadhi Shirikishi baina ya Serikali na wananchi wanaoishi na kuzunguka katika hifadhi hiyo.
Akizungumza na Jarida hili, Afisa Misitu Mkuu wa Hifadhi hiyo, Angyelile Sousa alisema, Serikali kupitia Wakala wake wa Huduma za Misitu (TFS) imewekeana Makubaliano ya kuhifadhi Msitu huo na vijiji 21 vinavyozunguka hifadhi hiyo. Vijiji vinne kati ya hivyo ambavyo ni Shebomeza, Mlesa, Chemka na Mikwinini vimo ndani ya Hifadhi hiyo Asilia.
Sousa alisema katika mfumo huo kila kijiji kimeunda kamati ya uhifadhi wa mazingira ambazo zinashirikiana kwa karibu na uongozi wa hifadhi hiyo kwenye shughuli za uhifadhi ikiwemo ulinzi wa rasilimali zilizomo.
Alisema kuwa makubaliano hayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa wananchi wa vijiji hivyo wameelimishwa na kuuelewa umuhimu wa hifadhi hiyo ambayo ina faida kubwa kwao, kwa Serikali na kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tanga.
Aliongeza kuwa mfumo huo umesaidia kuimarisha uhifadhi katika Msitu huo ambapo matukio ya moto yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa ikiwa na pamoja na shughuli za uharibifu wa mazingira kwa ujumla.
Akielezea faida za hifadhi hiyo alisema, Amani ni chanzo kikuu cha Maji yanayotumika katika Jiji la Tanga ambapo vyanzo vyake vinapeleka maji katika mto Zigi unaopeleka maji hayo Jijini humo. Vijiji vyote 21 vinavyozunguka hifadhi hiyo pia vinanufaika na maji hayo.
Alisema kuwa faida nyingine inayopatikana katika hifadhi hiyo ikiwa ni sehemu ya makubaliano kwenye uhifadhi shirikishi ni mchango wa asilimia 20 ya mapato yanayotokana na utalii ambayo yanatolewa kwa vijiji 21 vinavyopakana na hifadhi hiyo kwa ajili ya kusaidia katika shughuli za maendeleo za vijiji hivyo.
“Katika sehemu ya makubaliano hayo wananchi wa vijiji jirani wanaruhusiwa kuokota kuni kavu zinazopatikana katika hifadhi hiyo, matunda, mbogamboga pamoja na dawa za miti shamba. Wananchi hao wanaruhusiwa kuingia hifadhini kwa umbali wa mita 100 kutoka maeneo yao ya vijiji kwa ajili ya shughuli hizo” alisema Sousa.
Aliongeza kuwa watu binafsi pia wananufaika na hifadhi hiyo kwa kuwekeza katika mahoteli yanayowapatia kipato. Wananchi pia wanaotembeza watalii katika hifadhi hiyo wananufaika na ajira ambapo huchukua asilimia 60 ya mapato ya kutembeza watalii (Tour Guiding Fees), asilimia 20 ikibaki hifadhini na asilimia 20 nyingine ikienda kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.
Akizungumzia vivutio mbalimbali vilivyomo katika hifadhi hiyo, Sousa alisema kuna vivutio vingi vya utalii vilivyohifadhiwa vizuri ikiwemo Misitu ya Asili na Wanyama mbalimbali kama vile Kima wa Bluu (Blue Monkey), Mbega Weupe na Weusi (Black and White Collabus), Nyoka, vinyonga pembe tatu (Three Hornes Chamelleon), vipepeo na ndege wa aina mbali mbali ambao baadhi yao husafiri umbali mrefu kutoka barani ulaya kwa ajili ya kukimbia baridi kali na kuzaliana katika hifadhi hiyo.
“Vivutio vingine vilivyopo katika hifadhi hii ni Maporomoko ya Maji (Water Falls) ambayo ni Derema, Chemka, Ndola na Pacha. Pia kuna vivutio vya Vilele vya Milima (viewpoints) kama Kiganga, Ngua, Makanya, Mbomole na Kilimahewa. Ukiwa katika vilele hivyo unaweza kuona Mji wa Korogwe na Jiji la Tanga kwa juu” alisema.
Mbali na vivutio hivyo, alisema kivutio kingine ambacho ni cha kipekee katika hifadhi hiyo ni aina ya Ua linaloitwa “Saintpaulia” ambalo lina rangi ya Zambarau “Violeth Color”, Ua hilo pia linatumika kama nembo ya hifadhi hiyo. Upekee wa Ua hilo ni kwamba likipandwa sehemu nyingine yeyote duniani hubadilika rangi yake ya asili, Tafiti mbalimbali zimefanywa ikiwemo kujaribiwa kupandwa nchini Ujerumani na kutoa majibu hayo hayo.
Pamoja na vivutio hivyo kivutio kingine katika hifadhi hiyo ni mashine ya kusagia unga iliyokuwa ikitumia nishati ya nguvu ya kusukumwa na maji miaka 1986 katika kijiji cha Kisiwani na mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati hiyo hiyo iliyotumiwa na Wakoloni wa Kijerumani katika Kijiji cha Chemka.
Akizungumzia aina za utalii katika hifadhi hiyo alisema, upo Utalii wa Picha (Photography), Utalii wa Kutizama Ndege (Bird Watching), Utalii wa Kuangalia viumbe hai Usiku (Night Watching), Utalii wa Kiutafiti (Reseach Tourism), Utalii wa kiutamaduni (Cultural Tourism) na Utalii wa Kutembea na Kupanda Milima.
“Kwa upande wa gharama za kutembelea hifadhi ya Amani kama kiingilio kwa Mtalii mmoja kutoka nje ya nchi ni Dola 10 za Kimarekani na Mtanzania ni Shilingi10,000. Kwa upande wa gharama za watembeza watalii wa nje ni dola 15 za Kimarekani” alisema.
Nae Afisa Misitu wa Hifadhi hiyo, Isack Bob Matunda akizungumzia idadi ya watalii waliotembelea hifadhi hiyo na mapato yaliyopatikana alisema “Mwaka wa fedha 2015/16 jumla ya watalii 545 walitembelea hifadhi hii na jumla ya mapato yote yaliyopatikana ni shilingi milioni 50. Aidha, mwaka huu wa fedha 2016/17 mwezi Julai-Agosti jumla ya watalii 121 wameshatembelea hifadhi hii na mapato ambayo yameshapatikana ni shilingi milioni 7.3”.
Akielezea changamoto za uhifadhi, Afisa Misitu Mkuu wa Hifadhi hiyo, Angyelile Sousa alisema zipo changamoto kidogo ikiwemo uchimbaji wa madini kwenye vyanzo vya maji, uharibifu mdogo wa misitu ikiwa ni pamoja na uchomaji moto katika ukanda wa chini na miundombinu mibovu ya barabara.
Post a Comment