Header Ads

Serikali ya TANZANIA na INDIA zakubaliana Kutekeleza Miradi ya Maendeleo

Na. Immaculate Makilika 

Serikali ya India na Tanzania zimesaini mikataba ya miradi ya maendeleo katika sekta za maji, kilimo, viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano na afya katika kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili ili kusaidia wananchi wake.

Mikataba hiyo imesainiwa leo, wakati Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi alipokuakifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mikataba wa kwanza uliosainiwa inahusisha mradi wa kusambaza maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akikagua gwaride la heshima mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu Leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakiimba nyimbo za mataifa ya India na Tanzania, leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Aidha, mkataba wa pili unahusisha mradi wa kusambaza maji Zanzibar ambao unatarajiwa kugharimu dola  za kimarekani milioni 92 ambapo mradi huo unatarajiwa kufikia miji 17 nchini na mkataba mwingine utahusisha mafunzo ya ufundi yatakayosaidia kuzalisha wataalamu mbalimbali.

“Lengo letu ni kusaidiana  na kuimarisha mahusianao yetu katika kukuza uchumi na kutengeneza fursa mpya za ajira kwa wananchi wetu” alisema Waziri Modi.


Waziri Modi aliongeza kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa biashara na hatimaye kukuza uchumi wa nchi hizo.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakiwasalimia na baadhi ya Watanzania waliojitokeza wakati Bw. Narendra alipowasili katika viwanja vya leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alisema Serikali India imekua na ushirikiano mzuri na Tanzania hasa katika masuala ya maendeleo ambapo imeweza kuwekeza nchini kiasi shilingi za Kimarekani dola bilioni 2.4 na kuzalisha  ajira 54,176.

Baadhi ya misaada iliyotolewa na Serikali ya India ni pamoja na  mashine ya vipimo vya ugonjwa wa kansa katika hospitali ya Bugando, itakayosaidia wakazi wa kanda ya ziwa na nchi nzima kwa ujumla pamoja na kuongeza na kuimarisha ushirikiano kati ya Shirika la viwanda vidogo vigodo la India kushirikiana na Tanzania katika kukuza viwanda vidogo na vya kati nchini.

Katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Serikali hiyo imeahidi kuleta wataalamu wao nchini Tanzania kwa lengo la kutengeneza program mbalimbali ili kuisaidia Tanzania katika masuala ya ulinzi wa mitandao pamoja na kutengeneza namna bora za ukusanyaji wa mapato ya nchi.

Katika masuala ya viwanda, Serikali ya India imeahidi kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu  zitakazotibu   magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria, figo na kisukari, ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza gharama ya kununua vifaa hivyo nje ya nchi.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa nchi ya India ina uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo hasa jamii ya kunde hivyo akawataka wakulima kutumia fursa hiyo kuzalisha mazao hayo kwa wingi.

“India inauhitaji wa tani 200 za mazao jamii ya kunde, wakulima mnatakiwa kuzalisha mazao hayo kwa wingi kwa vile tayari kuna soko la uhakika, na tutahakikisha madalali hawatakuwepo ili mkulima asikandamizwe” alisema Rais Magufuli.

Katika sekta ya uwekezaji nchini, India ni nchi ya tatu kwa uwekezaji Tanzania ikifuatiwa na Uingereza pamoja na China.


Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakipiga ngoma wakati Waziri Mkuu Narendra alipowasili katika viwanja vya Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alipowasili Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akifanya Mazungumzo na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alipowasili Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Tanzania na India wakiwa katika mazungumzo maalum Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari ambapo ameahidi kusaidia katika utekelezaji wa Miradi ya Maji katika Miji ya Dar es Salaam na Pwani, pia kusaidia katika kuendeleza sekta za Habari na Mawasiliano, Viwanda Vidogo vidogo na Vyakati, Kilimo, Afya na masuala ya Usalama nchini, Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akiongea na waandishi wa habari wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ambapo ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa nchi hiyo katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo na kumshukuru Bw. Narendra kwa utayari wa kusaidia utekelezaji wa Miradi mbalimbali nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Dkt. Aziz Mlima na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa India Bw. Amar Sinna wakionesha ramani inayoonesha maeneo ya Nchi yaliyozungukwa na bahari wakati wa Ziara ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akimshukuru Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kwa kufanya Ziara nchini Tanzania na kuahidi utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Maendeleo nchini wakati wa Chakula cha Mchana leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akiongea na baadhi ya wageni walioalikwa kwenye Chakula cha Mchana Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akisalimiana na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa chakula cha Mchana Ikulu leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wakigongesha Glasi kutakiana Kheri.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akisalimiana na akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba wakati wa chakula cha Mchana Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwaeleza jambo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (Katikati) na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, wakati wa Ziara ya Waziri Mkuu wa India Ikulu leo Jijini Dar es Salaam. 

(PICHA NA HASSAN SILAYO-MAELEZO)














No comments

Powered by Blogger.