Jiji la Mbeya Kuwachukulia Hatua Kali za Kisheria Wachafuzi wa Mazingira
Frank Mvungi-Maelezo.
Jiji la Mbeya kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuwatoza faini ya shilingi elfu 50 hadi laki 3 wale wote watakaobainika kuchafua mazingira katika jiji hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Habari wa jiji la Mbeya Bw. John Kilua kufuatia taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu kuwepo kwa baadhi ya madereva wa magari makubwa wanaofanya uchafuzi wa mazingira katika stendi ya Mwanjelwa.
Akifafanua Kilua amesema kuwa Jiji hilo lina mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa wananchi wote wanazingatia sheria na kanuni za usafi ili kuweka jiji hilo katika hali ya Usafi.
“Katika eneo la Mwanjelwa kuna vyoo vya kulipia na ni rai yetu kuwa watu wote watavitumia wakiwemo madereva wa magari makubwa ambao wanalalamikiwa kusababisha uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo”alisisitiza Kilua.
Kwa upande wake afisa mazingira wa Jiji hilo Bw. Januari Kazoba amewataka wananchi wote kuzingatia sheria na kanuni za usafi ili kuepuka mkono wa sheria.
Aliongeza kuwa ni vyema wananchi wakajenga utamaduni wa kuzingatia usafi kwa maslahi ya Taifa ikiwa ni moja ya hatua za kuunga mkono juhudi za Serikali.
Jiji la Mbeya limekuwa likiwahamasisha wananchi kushiriki katika mikakati ya kufanya usafi na kuliweka jiji hilo katika hali ya usafi ili kuepuka magonjwa ya milipuko yatokanayo na uchafuzi wa mazingira.
Post a Comment