Nishati ya uhakika inahitajika kwa ukuaji wa uchumi – Prof. Muhongo
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiongoza
kikao kilichoshirikisha watendaji kutoka kampuni zinazojishughulisha
na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi za Statoil na ExxonMobil
pamoja na Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya
Petroli Nchini (TPDC)
Meneja
Mkazi wa Kampuni inayojishughulisha na shughuli za utafutaji na
uchimbaji wa gesi na mafuta ya Statoil Tanzania, Øystein Michelsen,
(kushoto) akielezea shughuli zakampuni hiyo kwa Waziri wa Nishati na
Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia)
Meneja
Mkazi wa Kampuni inayojishughulisha na shughuli za utafutaji na
uchimbaji wa gesi na mafuta ya Statoil Tanzania, Øystein Michelsen
akisisitiza jambo katika kikao hicho.
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (mbele) akiongoza kikao
kilichoshirikisha watendaji kutoka kampuni zinazojishughulisha na
utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi za British Gas (BG), Ophir,
Pavilion pamoja na Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC)
Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa ili Tanzania iweze kuwa nchi
ya viwanda, nishati ya uhakika inahitajika na kutaka makampuni
kuwekeza katika uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi.
Profesa Muhongo aliyasema hayo
jijini Dar es Salaam katika nyakati tofauti alipokutana na
watendaji wa kampuni zinazojishughulisha na Utafutaji na Uchimbaji wa
Mafuta na Gesi pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini
na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) lengo likiwa ni
kupokea taarifa ya maendeleo ya miradi mbalimbali ya makampuni hayo.
Kampuni hizo zinazofanya kazi
kwa kushirikiana na Shirika la TPDC ni pamoja na British Gas (BG),
Ophir, ExxonMobil na Statoil.
Profesa Muhongo alisema kuwa
hakuna nchi yoyote duniani iliyopiga hatua kimaendeleo bila kuwa na
nishati ya uhakika ya umeme na kuwataka wawekezaji kuchangamkia fursa
kupitia gesi nyingi iliyogunduliwa.
Alitaja maeneo yanayohitaji
uwekezaji katika kuzalisha umeme kwa kutumia gesi kuwa ni pamoja na
Mtwara, Lindi, Somanga Fungu, na Mkuranga
Aliongeza kuwa viwanda 37
pamoja na vya sementi vinahitaji gesi na kusisitiza kuwa iwapo sekta
ya gesi itatumiwa ipasavyo inaweza kuchangia nchi kupiga hatua na
kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025
kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyosema.
Wakati huo huo Profesa Muhongo,
aliwataka watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi
zake kufanya kazi kwa kasi ili kuendana na kasi ya uwekezaji katika
shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta.
“Sekta ya gesi na mafuta ambayo ni mpya inahitaji umakini na kasi ili kuvutia wawekezaji zaidi,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Akizungumzia mikakati ya
serikali katika kuzalisha wataalam katika masuala ya mafuta na gesi
Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imekuwa ikitoa ufadhili kwa
wanafunzi katika ngazi za shahada za uzamili na uzamivu katika vyuo
vilivyopo nje ya nchi vyenye uzoefu katika fani hiyo, pamoja na
uanzishwaji wa programu hizo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Madini.
Alisema kuwa mpaka sasa kuna
idadi ya takribani wanafunzi 98 waliohitimu masomo hayo na kuziomba
kampuni hizo kuajiri wataalam hao ili wawe na mchango mkubwa kwenye
sekta ya gesi.
“ Nia ya Serikali ni kuwa na
wataalam wazawa ambao watanufaika kupitia uchumi wa gesi kwa kufanya
kazi katika viwanda vya kuchakata gesi na kuzalisha umeme unaotokana
na gesi,” alisema Profesa Muhongo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka
Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) Dk. James Mataragio
alisema kuwa shirika hilo limekuwa likishirikiana na kampuni hizo
katika hatua zote muhimu hususan katika kiwanda cha kuchakata gesi
asilia kimiminika (Liquefied Natural Gas) na kuongeza kuwa mpaka sasa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda limeshapatikana.
Alisema kuwa, Tanzania
inatarajia kuwa kitovu kikuu cha gesi barani Afrika kwani gesi nyingi
itakayozalishwa itauzwa katika nchi nyingine.
Aliongeza kuwa nchi kama
Uganda, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Zambia zimeonesha nia ya
kuhitaji gesi kwa ajili ya kuzalisha nishati ya uhakika kwa kuwa nchi
hizo zinatumia maji kuzalisha umeme ambapo uzalishaji wake hupungua
hususan wakati wa kiangazi kutokana na kupungua kwa kina cha maji.
Naye Meneja Mkazi wa Kampuni ya
Statoil Tanzania, Øystein Michelsen, alisema kuwa kampuni yake ipo
tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa miradi yake
inakamilika kwa wakati.
Alisema tangu kampuni hiyo
kuanza shughuli zake nchini, imekuwa ikishirikiana na Serikali kwa
kutoa ufadhili wa masomo katika masuala ya gesi na mafuta nje ya nchi
kwa wanafunzi wanaofanya vizuri.
Aliongeza kuwa kampuni ya
Statoil imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriliamali kwa wakazi wa mkoa wa
Mtwara ili waweze kushiriki katika uchumi wa gesi kupitia utoaji wa
huduma zake kwa Kampuni hiyo.
Post a Comment