SERIKALI YATOA TAMKO KUHUSU TIBA ASILI NA TIBA MBADALA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu akitoa uamuzi wa Serikali kuhusu Serikali kuhusu Tiba
Asili na TibaMbadala katika mkutano
wa waandishi ulifanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa
wizara hiyo.kushoto ni Waziri wa Wizara
hiyo, Ummy Mwalimu, ambapo ameleza kwamba watoa huduma hao ni lazima wasajiliwe
na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala
wakiwemo wasaidizi wao, vifaa wanavyotumia na dawa. Pia imetoa muda wa miezi mitatu
kwa mijini na vijijini miezi sita kutekeleza agizo hilo..
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,
Wazee na Watoto Dkt.Hamisi Kigwangalla akifafanua jambo kuhusu uamuzi wa Serikali kuhusu Tiba Asili na TibaMbadala katika mkutano wa waandishi
ulifanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo.kushoto ni Waziri wa Wizara hiyo, Ummy Mwalimu.
..........................................
Katika nchi yoyote ile uhuru usio
na mipaka ni jambo la hatari; lakini pia hakuna haki isiyo na wajibu.
Vivyo hivyo, katika huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala hapa nchini
kuna Sheria, Kanuni na Taratibu za Maadili zinazoweka masharti, uhuru na
mipaka; pia haki na wajibu wa kila mdau. Huduma za tiba asili na tiba
mbadala ni huduma zinazotambulika na Jamhuri yetu, watu wake na ina
thamani kubwa. Aidha, ni huduma inayotambuliwa na sayansi ya tiba ya
kisasa. Hata hivyo huduma hizo zimekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kuwepo kwa watoa huduma wasiozingatia Sheria, Kanuni na
Miongozo mbalimbali. Kutokana na hali hiyo na kutokana na ziara ya Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt.
Hamisi A. Kigwangalla (Mb) kwa Tabibu Juma Mwaka Juma tarehe 14/12/2015
na kufuatia uchambuzi uliofanywa na Wizara baada ya ziara hii, Wizara
imebaini changamoto zifuatazo:-
1. Huduma za tiba asili na au tiba mbadala zinatolewa na watoa huduma wasiosajiliwa na Mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria.
2. Uwepo wa vituo vinavyotoa huduma za Tiba Asili na au Tiba Mbadala bila kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria.
3. Kutolewa dawa kwa wagonjwa bila dawa hizo kusajiliwa na mamlaka husika.
4. Uingizaji na matumizi ya vifaa vya uchunguzi ambavyo havijasajiliwa na mamlaka zinazohusika, na
5. Utoaji wa matangazo bila ya kufuatwa kwa matakwa ya sheria,
Kanuni na Miongozo iliyopo. Aidha baadhi ya matangazo hayo yamekuwa na
taarifa zinazoweza kuleta madhara na kupotosha Umma wa Watanzania.
Ndugu Wananchi,
Kutokana na hali hiyo, Wizara itahakikisha kuwa huduma za tiba
asili na tiba mbadala zinatolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
Miongozo iliyopo. Lengo ni kuwezesha huduma za tiba asili na tiba
mbadala zinakuwa huduma rafiki na salama kwa watumiaji. Tunao wajibu wa
kuwalinda wananchi, vile vile tunaowajibu wa kuweka mazingira mazuri kwa
watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala ili kufanya shughuli zao
vizuri.
Hivyo kwa upande wetu Wizara itahakikisha kuwa:-
1. Baraza na sehemu inayosimamia huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala inakuwa na watumishi wa kutosha kwa mujibu wa Ikama.
2. Kunakuwa na Mpango Mkakati wa muda mrefu kuwezesha kufanikisha uboreshaji wa huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
3. Watoa huduma wote, vituo vyote vya kutolea huduma, dawa na vifaa na vifaa tiba vinavyotumika vinasajiliwa.
4. Utaandaliwa mwongozo wa mafunzo kwa watoa huduma wote nchini,
kuhusu namna ya kuweka kumbukumbu za wagonjwa, kutoa rufaa kwa wagonjwa
na kutengeneza dawa zilizo bora.
5. Kunakuwa na mawasiliano na Wizara zinazohusika na habari na
mawasiliano ili kuboresha utoaji matangazo yanayohusu Tiba Asili na Tiba
Mbadala.
6. Kunakuwa na mawasiliano na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Taasisi
za Utafiti ili kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
7. Tutafanya mabadiliko ya Sheria ili kuongeza kiwango cha
adhabu kwa watakaokiuka, na pia tunakusudia kuondoa Kanuni inayoruhusu
matangazo kwa idhini ya Baraza kwa sababu inaweka mianya ya matumizi
mabaya ya fursa ndogo ya matangazo inayotolewa.
Ndugu Wananchi,
Katika kufanikisha hayo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto inatoa maelekezo yafuatayo kwa watoa huduma na
jamii:-
1. Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kutoa huduma za tiba asili na au
tiba mbadala bila kusajiliwa. Ninalielekeza Baraza la Tiba Asili na Tiba
Mbadala kuhakikisha kuwa watoaji huduma wote wanasajiliwa kwa mujibu wa
Sheria:
(a) Mijini, (Majiji, Manispaa na Miji) – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi mitatu; kuanzia Januari 15, 2016 na
(b) Vijijini, Halmashauri zote zilizobaki – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari 15, 2016.
Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye puuza kujisajili katika kipindi hicho
2. Hairuhusiwi kuuza na au kugawa dawa yoyote ile ya tiba asili
au tiba mbadala mpaka iwe imesajiliwa na Baraza baada ya kuchunguzwa na
Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni salama na kupewa
kibali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
3. Hairuhusiwi kuendesha kituo cha kutolea huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila kukisajili.
4. Wizara inapiga marufuku kwa mtu binafsi au taasisi yoyote ile
kutumia kifaa au kifaa tiba chochote bila kukisajili TFDA na kupewa
kibali; na
5. Matangazo yote yanayohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala ambayo
hayajapitishwa na Baraza yamezuiliwa kuanzia leo tarehe 15/1/2016.
Wizara inavitaka vyombo vya Habari hasa Televisheni, Radio na Magazeti
kuzingatia Sheria na Kanuni za Tiba Asili na Tiba Mbadala inayozuia
matangazo ambayo hayajachunguzwa na Baraza. Ni wajibu wa vyombo vya
habari kujiridhisha na Mamlaka husika yaani Baraza kabla ya kutoa
tangazo lolote linalohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala. Wizara
itashirikiana na Mamlaka zinazohusika na habari na mawasiliano
kutekeleza agizo hili. Vile vile, hairuhusiwi kutoa elimu kwa umma
kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara kuhusu tiba asili na
tiba mbadala.
Ndugu Wananchi,
Katika kuwezesha ulinzi wa afya za wananchi, kila mmoja wote
alinde afya yake kwa kuhakikisha kuwa huduma anayopata ya tiba asili na
tiba mbadala ni kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Ni uhakika
uliowazi kuwa kwa pamoja tukiboresha huduma za tiba asili siyo tu
tutaboresha afya zetu bali pia tutaweza kuuza dawa na huduma hizo nje ya
nchi na kupata fedha za kigeni kupitia na hivyo kuboresha uchumi wa mtu
mmoja mmoja, jamii na nchi kwa ujumla.
Kwa pamoja tushirikiane kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini. INAWEZEKANA.
Ummy A. Mwalimu (Mb)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO
15 Januari, 2016
Post a Comment